The House of Favourite Newspapers

BREAKING: Mwendokasi Iliyoua 3 Manzese, Polisi Yanasa Watu 20 – Video

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia Madereva wa bodaboda 20 kwa kuharibu basi la Mwendokasi tukio lililotokea hivi karibuni maeneo ya Manzese na kusababisha vifo vya watu kadhaa.

 

Akizungumza na wanahabari mapema leo, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, amesimulia ajali hiyo iliyosababishwa na uzembe wa dereva wa bodaboda ambaye nae alipoteza maisha muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali.


Kufuatia tukio hilo Kamanda Mambosasa ametoa onyo kwa Madereva wa bodaboda kutopita kwenye barabara ya Mwendokasi na kubainisha kuwa tayari wameshaanza operesheni ya kupambana na vitendo hivyo.

 

Katika hatua nyingine Kamanda Mambosasa amewataka wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam kuchukua tahadhari kuelekea katika sherehe za krismas na kufunga mwaka ili kujiepusha na madhara yanayoweza kutokea.

HABARI NA DENIS MTIMA | GPL

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUPATIKANA KWA SILAHA 2 AINA YA S/GUN PUMP ACTION NA RISASI 17.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dsm mnamo tarehe 29 Nov 2018 majira ya 10 :30 alfajiri huko maeneo ya Kinyerezi Kanga lilifanikiwa kukamata silaha mbili aina ya Shortgun Pump Action zenye namba za usajili P-913581 TZ CAR 76456 na P- 625302 TZ CAR 76467 pamoja na risasi kumi na saba.

Silaha hizo zilipatikana zikiwa zimetelekezwa kwenye mfuko wa plastiki mweusi na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi ambao hufanya matukio mbalimbali ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dsm linatoa wito kwa watu wote wanaomiliki silaha isivyo halali na kuzitumia katika

matukio ya kihalifu wazisalimishe haraka sana silaha hizo katika kituo chochote cha Polisi kabla hawajakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwani oparesheni ya kuwasaka wahalifu wanaotumia silaha ni endelevu.

 

KUKAMATWA KWA MENO YA TEMBO VIPANDE 20 NA WATUHUMIWA WATATU (3)

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam mnamo terehe 10 Disemba 2018 majira ya saa 3 : 45 usiku huko maeneo ya Kigogo fresh Ukonga, Polisi walifanikiwa kukamata vipande 20 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Tsh Millioni 87. Awali Polisi walipokea taarifa kuwa kuna watu wanaojihusisha na biashara hiyo ya nyara za serikali ndipo Polisi waliweka mtego na kufanikiwa kukamata watuhumiwa watatu wakiwa na vipande hivyo, watuhumiwa hao ni kama ifuatavyo ;

  1. SALEHE IDDI miaka 57, mfanyabiashara, mkazi wa vingunguti. 2. WAZIRI IBARAHIMU miaka 40, mfanyabiashara, mkazi wa 3. BERTHA NELSON miaka 38, mfanyabiashara, mkazi wa Yombo.

Watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa kwa kushirikiana na maofisa wa maliasili na utalii na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

JESHI LA POLISI KANDA MAALUM DSM KUIMARISHA ULINZI KATIKA MAENEO YOTE YA JIJI LA DSM KUELEKEA SIKUKUU ZA MWISHO WA MWAKA.

 

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya DSM kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka limeimarisha ulinzi maeneo yote ya jiji hususani katika taasisi mbalimbali za fedha (benki),maduka ya kubadilishia fedha za kigeni na sehemu zenye mkusanyiko wa maduka mengi kama Mlimani City, Quality Plaza, City Mall n.k

 

Ndugu wanahabari kama mnavyofahamu katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka kumekuwa na baadhi ya watu ambao hujitafuta kipato kwa njia isiyo halal kwa kufanya vitendo vya uhalifu,hivyo kutokana na hali hiyo Jeshi la Polisi Kanda Maalum limejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba hakuna tukio lolote la uhalifu litakalojitokeza katika kipindi hiki cha maandalizi ya Christmas na mwaka mpya.

Wananchi wasiwe na hofu yoyote pindi watakapoona kuna Idadi kubwa ya askari wakifanya doria katika maeneo

mbalimbali ya jiji la Dsm na badala yake watoe ushirikiano kwa kutoa taarifa za wahalifu kwa kupitia namba za simu zifuatazo-:

 

  1. SACP LAZARO MAMBOSASA- 0715 009 983 KAMANDA KANDA MAALUM
  2. ACP SALUM HAMDUNI- 0715 009 980 RPC ILALA
  3. ACP JUMANNE MULIRO- 0715 009 976 RPC KINONDONI
  4. ACP EMMANUELI LUKULA- 0715 009 979 RPC TEMEKE

 

JESHI LA POLISI KANDA MAALUM DSM LINAWASHIKILIA MADEREVA BODABODA 20 KWA UHARIBIFU WA BASI LA MWENDOKASI

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dsm linawashikilia madereva bodaboda 20

Kwa tuhuma za kulishambulia basi la mwendo kasi lenye namba T 155 DGW na kusababisha uharibifu mkubwa wa basi hilo.

Mnamo tarehe 8 Dec 2018 majira ya 08:15 usiku huko eneo la Manzese Tiptop, pikipiki yenye namba za usajili MC 964 BYN ikiwa inapita katika barabara ya mwendokasi iligonga basi la mwendokasi na kusababisha vifo vya watu wawili papo hapo ambao ni abiria wa pikipiki hiyo huku dereva

akijeruhiwa vibaya na kukimbizwa hospitali na baadaye alifariki akiwa anaendelea kupatiwa matibabu.

Baada ya ajali hiyo kutokea madereva bodaboda wanaopaki kandokando ya barabara hiyo walianza kumshambulia dereva, abiria na basi kwa mawe na kusababisha uharibifu wa gari hilo.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dsm linatoa onyo kali kwa madereva wote wa vyombo vya moto hususani pikipiki kuacha mara moja kutumia barabara za mabasi ya mwendo kasi ili kuepusha ajali ambazo zinaepukika na kugharimu maisha ya watu.

Hivyo Jeshi la Polisi linatangaza oparesheni kali ya bodaboda zote zinazopita katika barabara za mwendokasi.

 

L.B. MAMBOSASA– SACP

KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM DAR ES SALAM.

11.12.2018

Comments are closed.