Bulaya: Mipango ya Serikali ni Mizuri Lakini Fedha Hazitoki
Bunge la Tanzania linaendelea Mjini Dodoma ambapo zamu hii ni zamu ya kujadili bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2025/26 ambapo miongoni mwa waliochangia bajeti hiyo ni Mbunge wa Viti maalum Esther Bulaya ambaye ameeleza masikitiko yake na kuwataka wabunge wenzake kusimama kidete dhidi ya Wizara ya fedha, kuhakikisha inatoa fedha zinazopitishwa na Bunge kutekeleza miradi na mipango mbalimbali ya Wizara nyeti zenye kugusa maisha ya watanzania wengi.
Bulaya katika sehemu ya Hotuba yake ameeeleza;
“Mbali na mipango mizuri, Bajeti ya Kilimo kutoka Bilioni 200 mpaka Trilioni 1.2, pesa hazitoki zote. Simuoni Waziri wa fedha hapa, kazi yetu sisi ni kuibana Wizara ya fedha kupeleka pesa kwenye maeneo nyeti yanayogusa watu wengi. Leo bajeti ya mwaka huu tusingezungumzia tena Shilingi Trilioni 1.2, ingetoka yote tungewaza kuongeza iende ikasaidie wizara ya Kilimo.
Tulipitisha mwaka jana Trilioni 1.2 imetoka Bilioni 664 sawa na 53% kwanini sasa miradi ya umwagiliaji utekelezaji wake usiwe asilimia 28? Kwanini miradi mingi ya kilimo isikwame? Kwasababu hakuna pesa za kutosha. Kuna maeneo ambayo yanagusa watu wengi kwenye nchi hii, kilimo tunasema kinaajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania, huko tunatakiwa tuweke pesa za kutosha, unapozungumzia wizara ya afya pesa zinatakiwa ziende za kutosha, unapozungumzia Wizara ya maji, pesa zinatakiwa ziende za kutosha- kuna maeneo ya kimkakati yanagumza mtanzania mdogo lazima tuweke pesa za kutosha.
Haya leo hawa wana ndoto za kumsaidia mkulima mdogo, hatuwapelekei pesa ya kutosha, hiyo ndoto itatekelezwa vipi? Tunapeleka asilimia 53? Serious? Si bora ingefika hata asilimia 70 au 80?, asilimia 53 kweli? niombe wabunge wenzangu lazima tuibane Wizara ya fedha ili haya malengo mazuri yatimie”- amesema @bulayaester Mbunge wa Viti maalumu.