
Dar es Salaam, Julai 16, 2025 – Mtangazaji mahiri na maarufu nchini, Diva Gissele Malinzi, anayefahamika pia kama Diva The Bawse, ameaga rasmi kituo cha Wasafi Media baada ya kulitumikia kwa kipindi cha miaka minne.
Kupitia ujumbe wake wa kuaga alioutoa mapema leo, Diva amesema kwa heshima kubwa na moyo wa shukrani kwamba tayari ametuma barua rasmi ya kujiuzulu na kwamba anaanza ukurasa mpya wa maisha yake kitaaluma na kibinafsi.
“Kwa moyo uliojaa shukrani na upendo, nataka kusema rasmi asanteni na kwaherini ninapoaga rasmi nafasi yangu ndani ya Wasafi Media. Nimetuma barua ya kujiuzulu mapema asubuhi ya leo,” ameandika Diva.
Diva amekuwa mtangazaji wa kipindi maarufu cha usiku Lavidavi, ambacho kwa muda mrefu kimejipatia umaarufu mkubwa kwa kuibua mijadala ya mapenzi, uponyaji wa kihisia, ucheshi, na mazungumzo ya wazi yenye kugusa hisia za watu wengi.
“Kipindi cha Lavidavi kimekuwa moja ya sura nzuri kabisa kwenye kazi yangu ya utangazaji. Tulijenga nyumba ya hadithi halisi za mapenzi, ujasiri, uaminifu, na upendo wa kweli. Kila kipindi, kila sauti ya msikilizaji, kila ujumbe – kilikuwa sehemu ya moyo wangu, na nitabeba kumbukumbu hizo daima,” ameandika.
Aidha, Diva hakusita kuwashukuru wafanyakazi wenzake wote wa Wasafi Media wakiwemo watayarishaji, timu ya kidijitali, wahandisi wa sauti, menejimenti, na viongozi kwa ushirikiano na msaada waliompa katika kipindi chote alichokuwepo.
“Kila nafasi, kila msaada na kila kumbukumbu mliyonipa imenijenga na kunifanya kuwa bora zaidi,” amesema kwa moyo wa shukrani.
Akitafakari kuhusu hatua hiyo, Diva amesema maisha ni misimu, na sasa anapiga hatua nyingine mbele, akisisitiza kuwa huu si mwisho wa safari yake bali ni mabadiliko ya sura ya maisha yake.
“Maisha ni misimu – na sasa ninaingia kwenye msimu mpya. Huu si mwisho wa milele, bali ni kupumzika kwa heshima kwenye ukurasa mmoja huku nikigeuza ukurasa mwingine mpya. Popote nitakapokwenda, roho ya Lavidavi itaendelea kuishi,” amehitimisha.
Diva ameacha ujumbe mzito kwa jamii, akiwasihi waendelee kuamini katika nguvu ya mapenzi, kuponya mioyo, na kupenda bila kuchoka.
“Endeleeni kupenda, endeleeni kuponya, na zaidi ya yote – msikate tamaa kuamini katika mapenzi.”
Kwa sasa haijafahamika rasmi ni hatua gani inayofuata kwenye safari ya Diva kitaaluma, lakini mashabiki wake wanaamini kuwa bado ataendelea kung’ara popote atakapokwenda.