Dkt Mwigulu Aagiza Ziundwe Timu Za Mikoa Za Wakaguzi Wa Miradi – Video

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amemwagiza Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI) awaandikie barua Wakuu wote wa Mikoa ili waunde timu za ukaguzi wa majengo na miradi kwenye mikoa yao kama njia ya kukabiliana na wakandarasi wanaokiuka makadirio ya gharama za ujenzi (BOQ) wa miradi ya Serikali.
“Yuko Mhandisi ambaye huwa anakagua miradi wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru. Wakuu wa Mikoa wote wawe na timu za vijana wa aina hiyo, ili wasiuziwe mbuzi kwenye gunia. Iwe ni utamaduni wa Serikali kufanya ukaguzi wa aina hiyo,” amesema Waziri Mkuu.

Ametoa agizo hilo Jumapili, Desemba 21, 2025 wakati akizungumza na viongozi na wananchi wa Wilaya za Ruangwa na Nachingwea, mkoani Lindi akiwa katika ziara ya siku tatu ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani humo.
Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Waziri Mkuu amesema kuna baadhi ya miradi ambayo wakandarasi wake hawafuati BOQ. “Unakuta BOQ inataka nondo za mm 16 lakini mkandarasi anaweka za mm 12. Kuna mahali zinatakiwa nondo sita, yeye anaweka nondo nne. Jengo likikamilika, huwezi kuona na kulinganisha makubaliano ya BOQ. Nimeelekeza kila mkoa uwe na timu ya wataalamu wa kukagua miradi ya Serikali.”
“Mikoa yote wawe na vitengo hivi na wawe pia na vifaa vya kuchunguza majengo na miradi mingine badala ya kusubiri uchunguzi unaofanywa wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru. Vitengo hivyo kazi yao ya kila siku ni kufuatilia miradi ili kubaini maeneo ambako Serikali imetoa fedha na hazijatumika vizuri ili tuweze kuchukua hatua,” amesisitiza.

