The House of Favourite Newspapers

Dkt. Wilbroad Slaa amerejea Chadema, Tundu Lissu Ampokea

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, leo Machi 23, 2025 amemtangaza rasmi aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Willbroad Slaa kuwa amerudi ndani ya chama baada ya kutengana kwa muda mrefu.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Ruanda, Nzovwe, mjini Mbeya, Lissu ameeleza kuwa licha ya tofauti zilizowahi kutokea, CHADEMA imemsamehe Dkt. Slaa na kumkaribisha tena ndani ya chama.

“Kulikuwa na makwazano fulani, tukafarakana na kusemana vibaya. Sasa kama Dkt. Slaa anasema anataka kurudi, naomba yaishe. Tunasemaje hapana, nenda zako?” alisema Lissu mbele ya maelfu ya wanachama na wafuasi wa chama hicho.

Lissu amekumbusha mchango mkubwa wa Dkt. Slaa ndani ya CHADEMA, akieleza kuwa ndiye aliyemkabidhi kadi ya chama mnamo Julai 24, 2004.

Amesema kuwa wakati huo chama kilikuwa na wabunge wachache, lakini kupitia uongozi wa Dkt. Slaa, idadi hiyo iliongezeka maradufu hadi kufikia wabunge 72 wa CHADEMA na kufanya jumla ya wabunge wa Umoja uliofahamika kama UKAWA kufikia 117.

“Dkt. Slaa alikuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA aliyelitumikia chama kwa muda mrefu zaidi. Kipindi chake kilikuwa cha mafanikio makubwa kwa chama chetu kuliko kipindi kingine chochote,” alisisitiza Lissu.

Amefafanua kuwa Dkt. Slaa hakufukuzwa, bali aliondoka mwenyewe, na hivyo kurejea kwake hakuhitaji mchakato mgumu. Alisema kwamba kwa mujibu wa katiba ya chama, Dkt. Slaa angeweza hata kujiunga upya kupitia mfumo wa CHADEMA Digital, lakini ameomba kurudi hadharani kama alivyotoka, na hivyo chama hakina sababu ya kumkatalia.

Kuhusu wanachama wengine waliowahi kufukuzwa, Lissu dzazi kikatiba.

Amesema tayari chama kimepokea barua kutoka kwa wanachama wawili waliokuwa wamefukuzwa, huku akiwataka wengine kufuata taratibu kwa kuandika maombi kwa Katibu Mkuu.

Kwa hatua hii, inaonekana CHADEMA inapiga hatua katika maridhiano na kuimarisha safu yake kuelekea mustakabali wa kisiasa nchini.