The House of Favourite Newspapers

Dudu Baya Hajulikani Alipo Siku 60 Sasa!

0

Msanii mtata wa Bongo Fleva, Godfrey Tumaini almaarufu kama Dudu Baya (46), mkazi wa wilaya ya Kinondoni jijini Dar, ametoweka kwa takriban siku sitini (60) sasa katika mazingira ya kutatanisha, kiasi cha kujengeka hisia kuwa, huwenda ameuawa, RISASI MCHANGANYIKO linaripoti.

 

SI KAWAIDA YA DUDU BAYA

Dudu Baya ambaye pia kwa sasa anajiita Konki Master au Oil Chafu, umepita ukimya mrefu bila kusikika, jambo ambalo si kawaida yake, kwani anajulikana kwa ‘kushambulia’ watu mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii.

 

KIPINDI CHA KAMPENI

Zaidi ni Dudu Baya kutosikika wakati huu, ambapo wenzake wanaendelea kufunika kwa shoo za kukata na shoka kwenye kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu, utakaofanyika baadaye, Oktoba 28, mwaka huu, ilhali alikuwa tayari ameachia wimbo wake kuhusu Chama Cha Mapinduzi (CCM), unaokwenda kwa jina la Nakupenda CCM na kuahidi kuchanja mbuga na mgombea wa nafasi ya Urais wa chama hicho, Dk John Pombe Magufuli.

 

Hadi jana, Jumanne zilikuwa zimetimia siku 60, tangu Dudu Baya ametoweka katika mazingira yenye maswali lukuki, huku Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, likimtaka mwandishi wetu kufika kwenye ofisi zake zilizopo Oysterbay kwa ufafanuzi zaidi.

 

NI BAADA YA BINTIYE KUIBUKA

Maria Godfrey ni binti wa Dudu Baya, ambaye wiki iliyopita ndiye aliyefumbua macho ya wengi, baada ya kuibuka kwenye mitandao ya kijamii akilalamika kwamba, baba yake huyo haonekani, yapata miezi miwili sasa, hivyo kuomba msaada kwenye vyombo vya habari asaidiwe, ili baba yake apatikane.

Kwa mujibu wa Maria, baba yake amekuwa hapatikani tangu siku ya Agosti 13, 2020 na kwamba, amekwishamtafuta bila mafanikio.

 

“Msanii wa Bongo Fleva @ Dudubaya_Mamba_Oilchafu, kapotea tangu 13/8/2020 mpaka sasa hajulikani alipo, nilikuwa naomba vyombo vya habari viweze kumtangaza, ni mimi mwanaye @Konki_Maria,” aliandika Maria kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Gazeti hili liliperuzi kwenye ukurasa wa Dudu Baya wa Instagram na kubaini kwamba, mara ya mwisho kuonekana au kuposti, ilikuwa ni Agosti 12, mwaka huu kabla ya kupotea Agosti 13.

 

HOFU YA KUUAWA

Kwa mujibu wa kurasa za habari za mastaa kwenye mitandao ya kijamii, kila shabiki wa Dudu Baya amekuwa akionesha kuingiwa na hofu ya kuuawa na kumuomba Mungu, asipatwe na jambo baya kama hilo.

“Tumemmisi sana, Allah amnusuru maana bado tunamhitaji… “Tunamuombea huko aliko awe salama. “Mungu amlinde popote alipo… “Jamani Dudu, nilikuwa ninajiuliza tangu kampeni zianze, mbona sijamuona?

 

“Dudu Baya uko wapi jamani? Watoto wako wanakutafuta, tafadhali rudi nyumbani ukawaone… “Tunamuombea awe hai, kwa sababu ana bifu na watu wengi, inawezekana mmojawapo ametekeleza uhalifu dhidi yake…”

Ilisomeka sehemu ya maoni lukuki juu ya habari ya kupotea kwa Dudu Baya, huku wengi wakiwa na hofu, huwenda ameuawa!

 

SAA KADHAA KABLA

Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kwamba, saa kadhaa kabla ya kupotea kwake, alikuwa amewashambulia watu kadha wa kadha kupitia video zake zilizorushwa mitandaoni.

 

KAMANDA: NIPE NUSU SAA

Baada ya sakata hilo kuwa ndiyo habari ya mjini, gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Mussa Taibu ambapo aliulizwa juu ya kupotea kwa Dudu Baya na kama ana taarifa zozote, ambapo aliomba apewe muda wa nusu saa afuatilie.

“Sina taarifa za huyo msanii kukamatwa hapa kituoni kwangu, lakini nipe nusu saa nifuatilie kisha nitakujulisha,” alisema Kamanda Taibu.

 

ATAFUTWA TENA

Nusu saa baadaye, mwandishi wetu alimtafuta tena Kamanda Taibu ambapo alisema amefuatilia, lakini watendaji wake wamesema hayupo kituoni hapo.

 

MKUU WA MKOA NAYE

“Hebu nikumbushe tena, ulisema huyo msanii anaitwa nani? (mwandishi anamtajia jina). “Aaah! Sasa kwa bahati nzuri hapa nipo na RC (Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge) wangu, hebu ngoja nimuulize kama ana taarifa hizo,” alisema na kumuuliza Mkuu wa Mkoa, kisha akajibu; “Nimeongea na RC (Kunenge) hapa na watendaji wangu wote, naona hawajui kama yupo, naona tuendelee kufuatilia kwenye vituo vingine kama yupo.”

 

DUDU BAYA NI NANI?

Dudu Baya amezaliwa jijini Mwanza, mwaka 1974. Ni mtoto wa kwanza kati ya watoto 13 wa Mzee Tumaini. Wakati wa utoto, Dudu alitumia muda wake mwingi kushinda kanisani na alikuwa anapenda kuimba nyimbo za Injili. Mwaka 1997 alikwenda mkoani Morogoro kujiunga na chuo cha dini ili atimize ndoto yake ya kuwa padre.

 

Lakini baadaye, Dudu akageuka, akawa anakwenda Klabu ya Mango Garden iliyopo Morogoro mjini kwa ajili ya kujihusisha na muziki. Mwaka 1998, Dudu Baya aliingia rasmi kwenye muziki akitumia jina la Double G (Godfrey Ganster). Wakati huo pia alialikwa kwenye matamasha ya akina Sugu na Afande Sele.

 

Dudu Baya alikuwa anarap kwa kutumia biti za wasanii wa Marekani. Mwaka 2000, Dudu Baya alitumbukia jijini Dar ndipo alipotoa wimbo wake wa kwanza uliitwa Mwanangu Huna Nidhamu, aliorekodi kwenye Studio ya MJ Records chini ya Master Jay.

 

Dudu Baya aliachia abam yake ya kwanza ya Ni Saa ya Kufa, aliyozungumzia umalaya na Ukimwi, ambapo sasa alianza kuitwa kutumbuiza kwenye matamasha ya ndani na nje ya nchi. Mwaka 2001, Dudu Baya alitoa albam nyingine iliyokwenda kwa jina la Amri Kumi za Mungu.

 

Mwaka 2002 aliachia wimbo mkali wa Nakupenda Mpenzi, kisha aliachia Kurusumu, Sikutaka, Mpangaji na nyingine kibao. Baada ya hapo, Dudu Baya alianza kupata shoo kama zote kwenye nchi za Uganda, Kenya, Rwanda, Comoro, Zambia, Burundi na Kongo-DR.

 

Baada ya kuanguka kimuziki, miaka ya hivi karibuni, alianza kushambulia watu mbalimbali hasa mastaa wenzake, kiasi cha Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), kumfuta kwenye orodha ya wasanii nchini, kabla ya kufunguliwa tena.

 

Dudu Baya ambaye ni baba wa watoto wawili, amewahi kujiita Double G, Ngumi Jiwe, Kapafona, Mapafu ya Mbwa na kwa sasa anajiita Konki Master, Oil Chafu, Mamba na mengineyo.

Stori: Memorise Richard, Risasi

Leave A Reply