The House of Favourite Newspapers

FAHAMU AINA YA MAUMIVU YA KICHWA

0
aina ya MAUMIVU YA KICHWA
Maumivu ya kichwa.

 

DALILI za maumivu ya kichwa zinaweza kumsaidia daktari wako ajue nini kinachosababisha maumivu hayo hatimaye kujua matibabu yako yatakuwa vipi. Maumivu ya kichwa mara nyingi huwa hayasababishwi na sababu za hatari sana au hayamaaanishi kuna ugonjwa mbaya sana unaendelea mwilini, lakini wakati mwingine yanaweza kumaanisha kuna ugonjwa wa hatari mwilini unaohitaji matibabu ya haraka.

 

Kuuma kwa kichwa kunaweza kugawanywa katika makundi kutokana na visababishi kama ifuatavyo: Maumivu ya kichwa ya awali (primary headache) Maumivu haya husababishwa na kuongezeka kwa hisia za maumivu katika viungo vinavyotambua maumivu ndani ya ubongo. Maumivu haya ya awali hayamaanishi kuwa kuna ugonjwa unaendelea.

 

Mfumo wa kemikali katika ubongo, mishipa ya fahamu, mishipa ya damu ya nje ya fuvu ama misuli ya shingo na kichwa huchangia katika kusababisha maumivu ya kichwa ya awali. Baadhi ya watu wamebeba vinasaba vinavyosababisha wao kupata maumivu haya maishani mwao.

 

Aina hii ya maumivu ya kichwa nayo imegawanyika katika makundi makubwa mawili;

 

(1)MAUMIVU YA KICHWA YA MIGRAINE (MIGRAINE HEADACHE)

Aina hii ya maumivu ya kichwa ndiyo ambayo imeenea sana na watu wengi wanaosumbuliwa na maumivu ya kichwa ya mara kwa mara huwa na tatizo hili la migraine. Maumivu haya yanaweza kuwa ya upande mmoja; lakini yanaweza kuwa katika paji la uso pia na kusikika katika eneo lote la paji la uso, na shingo. Aina hii ya maumivu ya kichwa huwa ni ya “kichwa kugonga” (throbbing pain) na huambatana na dalili kama vile kichefuchefu na/au kutapika, kizunguzungu, macho kushindwa kuona vizuri, macho kuuma yanapoangalia mwanga.

 

Aina hii ya maumivu ya kichwa huzidishwa na kutembea au kujisogeza kwa namna yoyote, na mgonjwa hujisikia nafuu akipumzika hasa kulala. Kwa kawaida, maumivu haya huwa makali kwa muda wa saa moja hadi mbili na yanaweza kuchukua kati ya saa nne hadi 72.

 

Vitu ambavyo huweza kusababisha mtu mwenye tatizo la migraine kuanza kuumwa kichwa ni kama vile vinywaji vyenye kemikali ya caffeine au pombe, sigara, mawazo, uchovu, usingizi, hasira, kwa kinadada kama akiwa anakaribia siku zake, au kwenye siku zake, mwanga mkali na sauti kali ya chochote. Aina hii ya maumivu ya kichwa pia huwasumbua zaidi wanawake ambao wako katika umri wa kuweza kushika mimba ambao ndio wameanza kupata hedhi zao kipindi cha karibuni.

 

Pia, migraine huweza kurithiwa kutoka kwa wazazi kwa sababu mara nyingine husababishwa na vitu ambavyo viko kwenye vinasaba (genetics) vya uzao husika. DALILI Pia, aina hii ya maumivu ya kichwa mara nyingi hutanguliwa na ‘dalili za kabla’, ambazo hutokea kwa kati ya dakika 5-20, na hudumu si zaidi ya dakika 60; dalili hizi za kabla zinaweza kuwa kizunguzungu, kichefuchefu, mwili kukosa nguvu, n.k.

 

(2) MAUMIVU YA KICHWA YA ‘MGANDAMIZO’(TENSION HEADACHE)

Aina hii ya maumivu ya kichwa kwa kawaida huwa ni ya ‘kugandamiza au kukaza’ (pressing/tightening), na huwa yanatokea kwenye pande zote za paji la uso kuelekea utosini; na hayazidi pale mgonjwa anapotembea au kujisogeza (tofauti na migraine). Aina hii ya maumivu ya kichwa yanaweza kudumu kwa kati ya dakika 30 hadi siku saba na hayaambatani na dalili za kichefuchefu, kutapika, kizunguzungu kama ilivyo kwa migraine! Pia hakuna dalili za awali.

 

Mara nyingi maumivu haya huanza pale mtu anapokuwa na msongo wa mawazo; na huambatana na kukosa usingizi (insomnia). Maumivu ya kichwa ya upili (secondary headache) Aina hii ya maumivu ya kichwa husababishwa na tatizo lingine ambalo lipo ndani ya mwili na mgonjwa hupata maumivu haya kama matokeo ya tatizo hilo lingine mwilini.

 

DALILI Maumivu haya huambatana na homa, kupungua uzito, dalili za mfumo wa fahamu (kuchanganyikiwa, kuzimia, kupungua kwa hali ya ufahamu, macho kushindwa kuona, mwili au sehemu ya mwili kupooza), maumivu ya viungo na mifupa. Dalili nyingine ni kuishiwa damu.

 

Itaendelea wiki ijayo…

 

Baada ya Lissu Kuliamsha Dude, Serikali Yafunguka Sakata la Bombadier

Usipitwe na Matukio, Install ===>Global Publishers App

Sikiliza Hadithi za Mtunzi Eric Shigongo Hapa

Leave A Reply