The House of Favourite Newspapers

Haolewi? Hujui Sababu? SOMA HAPA!

KUOLEWA au kutoolewa ni majaaliwa ya Mungu lakini zipo sababu ambazo zinaweza kumfanya mwanamke akawa anatanga na njia kila siku bila kupata mtu wa kumuoa. Kila mwanaume anashindwa kumuoa kutokana na mwenendo wa maisha yake.

Ni vizuri sana kujitathimini kitabia ili utakapoona udhaifu wako basi uufanyie kazi na uweze kupata mtu sahihi wa kukuoa. Waswahili wanasema; afya yako inatokana na jinsi unavyokula.

Wakati mwingine hata aina ya ugumu wa kutoolewa unaoupitia kwenye uhusiano unatokana na jinsi wewe mwenyewe ulivyojiweka.

Ndugu zangu, wanawake wengi wamekuwa wakipoteza sifa za kuolewa kwa kukosa haiba ya kike. Mwanamke unapaswa kuuvaa uhusika wa kike. Mwanamke usiwe kama mwanaume.

Mwanamke kweli mtu akikukuona anajua kweli amekutana na mwanamke.

Haiba ya mwanamke si kuwa mzungumzaji sana kwa mwanaume hususan mwanaume wake. Mwanamke mwenye haiba ya kike ana heshima, mpole, mcheshi na mkarimu.

Anajua jinsi gani mume anapaswa kuheshimiwa. Anajua azungumze vipi na mwanaume. Azungumze nini na wakati gani.

Sio mwanamke unaoongea wee mpaka unakuwa kero kwa mwanaume hususan mwanaume wako anapokuwa na wanaume wengine. Mwanamke mwenye haiba ya kike anapomuona mwanaume wake yupo na wanaume wengine, si hodari wa kuzungumza eneo hilo.

Anajua pale si sehemu yake. Si mahali pa kuonesha ufundi wa kuzungumza. Hata kama ana hoja ya kuzungumza au kumkosoa mwanaume wake, hawezi kuzungumzia hapo. Atatafuta muda mzuri wa kuzungumza na mwanaume wake tena katika lugha rafiki.

Wanawake wengi hawaolewi kutokana na jinsi wanavyojiweka. Hawauvai ule uhusika wa kuwa mtu ambaye anakwenda kuwa mke au mama wa familia. Mwanamke anayejiandaa kuwa mke wa mtu anajua kuzingatia majukumu yake.

Anajua kwamba aishi vipi, avaaje. Sio mwanamke unavaa mavazi ya ajabuajabu, unaishi maisha ya kihuni kila siku unategemea nini? Mwanamke anayejiandaa na maisha ya heshima ya kuwa mke, anavaa mavazi ya heshima na anajiheshimu yeye mwenyewe

Mwanamke mwenye haiba ya kuwa mke ni mvumilivu wa mambo. Ana staha katika kuzungumza jambo. Anatambua utu ni nini. Anatambua shida na raha, si mtu wa kupenda tu maisha mazuri bali anatambua pia kuna nyakati za vipindi vigumu katika maisha.

Wanapokuwa kwenye nyakati ngumu, mwanamke mwenye haiba ya kike anatimiza wajibu wake sawasawa kwa kumtia nguvu mwenzi wake. Anatambua kwamba kuna kupanda na kushuka kwenye maisha. Kuna kupata na kukosa.

“Kama tumekosa leo, kesho tutapata. Usiwe na wasiwasi kwani maisha ndivyo yalivyo,” hizo ndio kauli za mwanamke anayejua thamani ya kuwa mke.

Wanawake wengi hawaolewi sababu ya kuwa na gubu. Wanawake ambao wanapenda kukasirikakasirika hovyo, kupenda ugomvi kila wakati au kusababisha kelele za kila wakati, hao mara nyingi hawaolewi.

Wanaishia kupuyanga muda mrefu maana wanaume hawapendi kero ndani ya nyumba. Wanachoshwa na mambo mengi ya maisha, wanatamani zaidi kupata faraja kwa wenzi wao na si kuongezewa kelele na wanawake wao.

Wanawake wengi pia hawaolewi sababu hawana hofu ya Mungu. Wanajiweka mbali na Mungu, wanaishi maisha ya ajabuajabu halafu mwisho wa siku wanaishia kukufuru Mungu.

Ni matumaini yangu mtakuwa mmenisoma. Tukutane wiki ijayo.

Comments are closed.