visa

HATA ‘SINGLENDI’ NI NGUO YA NDANI

HALOOOOO EEEHHHH wanakwambia raha ya tembele liwe na mafuta mengi, upo nyonyo! Mjini mjini tu kama umezoea maghorofa wenzako tumezoea kujulikana! Heee heeeeiyaaa!  Shoga kuna wanaume wengine kama bati bovu muda wowote upepo ukija linatoka, mvua ikinyesha hapakaliki, chefuuuuu! Jamani usingizi wa mtoto hauna mahesabu, uongo shoga?

Usinione nimefurahi ukajua leo Anti Naa hana kitu, hana minyoooshooo! Shuuuutu! Kwa taarifa yako tu shoga yangu leo nazungumzia tabia ya baadhi ya wanawake wenzangu kuchagua nguo za kumpa msichana wa kazi ‘hausigeli’ kufua. Utakuta mama ndani asubuhi anamwita msichana wake, anampa suruali, mashati, fulana na sing’lendi anamwambia fua hizi huku akiacha ‘kufuli’ tu kwamba, atafua yeye mwenyewe.

Kuna wengine nikisema singlendi nimewaacha kabisaaa hawaelewi hata ndiyo nini! Shoga hapa nazungumzia singlendi zile ambazo akina baba huzivaa ndani ya mashati tu na si zile wanazovaa nje kama wanamichezo. Zile ambazo kazi yake sahihi ni kuziba sehemu kubwa ya kifua toka mabegani hadi tumboni. Ina mikono ya kukatisha mabega, upo?

Vazi hili huwasaidia akina baba au wanaume kwa ujumla kusitiri mashati kulowa jasho inapotokea kuwepo kwenye joto kali. Lakini pia huchangia uimara wa vazi la nje katika mtoko. Ngoja nikung’ate tu sikio shoga yangu maana najua mimi na wewe tena kama kiberiti na jiko! Shoga katika nguo wanazovaa wanaume, singlendi imewekwa kwenye kundi la ‘nguo za ndani’ au kwa lugha ya kigeni ‘underwear’. Kwa akina baba mnaonunua nguo hizo madukani au kwa machinga, ukiangalia maandishi ya utambulisho kwenye karatasi wanazofungia, yanasomeka; underwear’.

Sasa tukirudi kwenye maisha ya majumbani mwetu, wewe mwanamke mwenzangu ni kwa nini umpe msichana wako wa kazi, nguo ya ndani ya mumeo ili akufulie? Maana hapa tumeona underwear si kufuli tu, hata singlendi. Inamhusu vipi dada wa kazi kwa mfano?! Tambua kwamba, kama una mazoea ya kumpa dada wa kazi singlendi za mumeo afue, basi mpe na kufuli nazo afue kwani zote ni kufuli ambazo hatakiwi kuona na mahali pake sahihi ni chumbani tu.

Vinginevyo, anzeni mazoea ya kufua singlendi wenyewe ili kuwatunzia heshima waume zenu kwani wasichana wa kazi wanapofua nguo hizo na kuziona zimefumuka au kuchanika ni sawa na kuona kufuli ikiwa hivyo. Mimi hata nguo nyingine za mume wangu nafua mwenyewe, msichana wa kazi hazimhusu kwani tabia ya kumwachiamwachia yeye iko siku mtajikuta mmekuwa wake wenza! Ohoo!

Lakini nikija kwenu akina baba na nyie acheni tabia ya kuvaa singlendi mbele za watu. Utamkuta baba ameamka chumbani, anavaa bukta na juu singlendi halafu anatoka mpaka nje, wengine mpaka dukani kwa Mangi. Hapo mjue ni sawa na mtu aliyetoka nje akiwa amevaa kufuli tu bila bukta na kuanza kuzurura, aibu gani hiyo!

Nimeona niliseme hili kwani mimi najifunza mambo mengi kila kukicha ndiyo maana kwenye kazi zangu za kuwafunda warembo wanaokwenda kuanza maisha ya ndoa ili kuepukana na tabia kama hizi huwa wananielewa sana! Kwa leo niishie hapa shoga yangu, asanteni kwa kunisoma. Ni mimi Anti Naa ukipenda waweza kuniita Anti Nasra au Shangingi Mstaafu!
Toa comment