Hatari ya penzi linaloanza kwa kasi na ‘nguvu ya soda’

NI wiki nyingine tulivu kabisa tunakutana tena kupitia safu hii nikiamini kwamba umzima buheri wa afya na unaendelea vyema na shughuli zako za kila siku kama kawaida.  Mimi namshukuru Mungu ambaye amenipa uwezo wa kuandika makala haya ambayo naamini yatakuwa ni yenye faida kwa wale watakaobahatika kuisoma.

Ni kuhusu mapenzi ambapo leo nataka kuzungumzia yanayosababisha penzi la wawili waliokaa kwa muda mrefu linavyoweza kuisha nguvu na kufa kabisa endapo hatua za makusudi za kuliboresha hazitachukuliwa.

Kimsingi ipo hali ya kujisahau baada ya wapenzi kuwa katika uhusiano kwa muda mrefu, haieleweki kama ni tabia ya mtu ama uhalisia wa mambo kwa sababu ukweli ulio wazi ni kwamba, mwanzo wa uhusiano wengi hujitahidi kufanya mambo ambayo yatamfurahisha mpenzi wake lakini kadiri siku zinavyosogea, penzi huanza kuchuja.

Kama huamini katika hili, peleka kumbukumbu zako kipindi kile ambacho ndio jamaa kaamua kuweka hisia zake wazi kwamba anakupenda na sasa hivi, utagundua ipo tofauti kubwa sana. Huenda mlikuwa na desturi ya kununuliana zawadi kama maua, kadi, chokoleti tabia hiyo itapotea, hakuna kati yenu atakayekumbuka kitu hicho, ni wachache sana ambao wanakwenda na wakati ndiyo huendelea kuzingatia hilo.

Kuna wale ambao walikuwa na tabia ya kukutana kila mara kimapenzi kabla ya kuoana, enzi hizo kila mmoja alitaka kumuonesha mwenziye namna gani alivyo fundi wa ‘kuyarudi’ ndani ya uwanja wa mapenzi lakini yale manjonjo huadimika kabisa.

Kawaida yenu ilikuwa kubadilisha hoteli kwa ajili ya chakula cha jioni lakini tabia hiyo hutoweka, labda kila wiki ilikuwa lazima muende ‘out’ mara tatu katika kumbi tofauti za starehe na kufurahia mapenzi yenu, hali hiyo itabaki historia tu. Hujawahi kumsikia msichana anasema; “Enzi zile kila wiki ilikuwa lazima twende beach na honey wangu lakini siku hizi nikigusia tu kwenda huko ni ugomvi.”

Wapenzi wengine walikuwa na kawaida ya kupitiana wakati wa lunch na kwenda kujumuika pamoja nyakati za mchana lakini taratibu kila mmoja ataanza kuiacha tabia hiyo na kusingizia kazi nyingi!

Pamoja na hali hiyo mabadiliko yote yana tiba, lazima ufahamu kuwa endapo ulikuwa na gerentii ya kutoka na mwandani wako ijenge na uidumishe, ukisitisha mtaanza kulaumiana ndani kwa ndani kabla ya watu wa nje kuwacheka na kusema ‘kumbe ilikuwa nguvu ya soda!’

Aidha kuna mabadiliko ya kimaslahi, pengine mtu na mpenzi wake wameketi na kuona wanatumia pesa nyingi viwanja, kwa hiyo wanaamua kupunguza au kuacha ili kujenga maisha bora kama familia, si unajua tena mnapokuwa na malengo ya kimaisha zaidi.

Kimsingi mabadiliko mengi ni yale yanayoleta dosari, haiwezekani upunguze kumridhisha mpenzi wako, haipendezi upunguze usafi, haivutii uache yale manjonjo yaliyokuwa ‘yakimkong’oli’ mpenzi wako mpaka akawa anajiapizak utokukuacha. Yapo mabadiliko mengi, lakini zaidi tujirekebishe tukumbuke kwamba baadhi ya vitu tulivyokuwa navyo ndivyo vilivyo wavutia wapenzi wetu na kukubali kufunga nasi ndoa, tukiacha tunakuwa tunawakatili.

Tuache kutengeneza mapenzi yenye nguvu ya soda, huo ni usanii ambao umewaathiri wengi waliokuwa wakidhani wamepata kwa mbwembwe zile za awali lakini baadaye wakaja kubaini wamepatikana baada ya mbwembwe kuisha.


Loading...

Toa comment