Heri Niwe Peke Yangu – 04

“Baada ya Jonathan kuzima taa, alifunga mlango wa chumbani na kuniaga kuwa anatoka kidogo angerejea baadae. Hakika sikupoteza muda nilifanya kile alichoniomba na baada ya saa moja, alirudi nyumbani na kuniomba niondoke mara moja nyumbani kwake. Wakati huo alionekana mwenye hasira sana na tayari alikuwa amelewa kupindukia. Niliondoka na kumuacha akiwa analia kwa uchungu huku akiwa amekukumbatia.

“Kadri muda ulivyoanza kusonga, Jonathan alianza kunichukia. Yale mahusiano yetu mazuri yalianza kupungua hata uaminifu wetu katika biashara ulianza kufifia. Kitendo cha kukujua kiliufanya urafiki wangu na Jonathan kuingia matatani. Mambo yalikuwa mabaya zaidi baada ya miezi tisa kutimia kwani malengo ya Jonathan hayakutimia kama alivyotaka.

 

“Nakumbuka ilikuwa ni alfajiri moja hivi, nilipokea simu kutoka kwake akiniambia kuwa ananichukia sana na wala haitaji kunifahamu tena kwani lengo lake halikutimia kama alivyotaka badala ya wewe kujifungua mtoto wa kiume, ulijifungua mtoto wa kike ambaye ndiyo huyu Elizabeth. Sikuridhiswa na kauli yake niliondoa gari langu haraka na kuelekea nyumbani kwake pasipo kujali uwepo wako. Nilipofika getini nilimpigia simu kuwa nipo nje, alipaniki sana na kutoka nje haraka. Aliniomba nisiingie ndani akanisihi nitangulie katika hoteli ya Gold Crest tuweze kufanyia mazungumzo hapo. Niliheshimu kauli yake na kufanya hivyo.

 

“Baada ya nusu saa aliwasili na tukaanza mazungumzo. Aliniambia hataweza kunipatia kiasi cha milioni 10 kama alivyoniahidi kwani hayakuwa makubaliano yetu wewe kujifungua mtoto wa kike bali alihitaji awe wa kiume. Nilikasirika sana wala sikutaka kumwelewa alichosema ilibidi nimuombe anipe walau nusu ya kiasi hicho lakini bado alikataa na kuniambia niende zangu kazi aliyonipa imenishinda.

 

“Nilimuomba endapo mwanangu Elizabeth akikuwa basi nije kumchukua ila bado alikataa na kuniambia mimi na yeye hatuna biashara yoyote tena na hivyo niondoke na kusahau kila kilichotokea. Kitendo hicho kilijenga uadui kati yangu na Jonathan kwani nilimchukia sana na wala hakuna aliyekuwa akimsemesha mwenzake na hatukushirikiana tena kwenye biashara zetu kama ilivyokuwa mwanzo.

 

“Baada ya mwaka mmoja nilipata taarifa kutoka kwa rafiki yangu wa karibu kuwa wewe na Jonathan mmeachana. Hakika nilifurahi sana kusikia hivyo nikaona hiyo ndiyo nafasi pekee ya mimi kuwa na wewe na kuweza kumlea mwanangu Elizabeth. Na ndiyo maana baada ya wewe kuachana na Jonathan, haikupita muda mrefu nilikutafuta na kuanza kujenga urafiki na hatimae tukawa wachumba na sasa kilichobaki ni kukamilisha ndoa yetu,” Felix alimaliza kumsimulia Abigail mkasa mzima uliomuhusu mtoto Elizabeth ili kumhakikishia kuwa siyo mtoto wa Jonathan bali ni mtoto wake.

 

Abigail alilia sana bila kukoma alimuomba Felix wapange siku ambayo wangeweza kukutana wote watatu yaani yeye, Jonathan na Felix ili ajihakikishie kama hayo ambayo Felix amemsimulia kuhusu mtoto Elizabeth ni ya kweli.“Kama umeshindwa kuniamini mimi, basi ila huwezi kunikutanisha na huyo Jonathan kwani ni adui yangu mkubwa labda kama atanipa pesa yangu milioni 10 aliyoniahidi,” kitendo cha Felix kukataa ombi la Abigail, kilimfanya Abigail akasirike zaidi na kuamua kuondoka kuelekea nyumbani kwake. Akiwa ndani ya gari lake alijaribu kumpigia simu Jonathan lakini simu yake haikupatikana kwa wakati huo.

 

Alipofika nyumbani, alipumzika na ilipofika saa mbili usiku kama ilivyokuwa kawaida yake aliwasha runinga kutazama taarifa ya habari. Kitendo cha yeye kuwasha tu runinga alisikia habari ya kuwa, “Mfanya biashara maarufu wa jijini Mwanza anayejulikana kwa jina la Jonathan amekutwa pembezoni mwa Ziwa Victoria maeneo ya Bukumbi akiwa hajitambui kabisa na mwili wake ukiwa na majeraha makubwa sana. Akiripoti kutoka kituo cha polisi, mwana habari wetu amesema jeshi la polisi bado linaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha tukio hilo. Kwa sasa mfanya biashara huyo yupo hospitali ya Bugando akiendelea na matibabu japo hali yake ni mbaya sana,” Abigail alichanganyikiwa sana baada ya kusikia taarifa hiyo. Alimpigia simu Felix kumuelezea kuhusu hiyo habari mbaya ila Felix hakuonyesha kujali saana. “Tulia mpenzi wangu acha kupaniki subiri kukuche utaenda kumuona hospitali kesho sasa hivi ni usiku sana,” alijibu Felix.

 

Abigail hakutaka kumuelewa kabisa Felix, alitoka nje na kuwasha gari lake kisha alielekea Bugando. Hakuamini kile alichokiona baada ya kufika pale hospitalini. Jonathan alikuwa amejeruhiwa mwili mzima. Watu wengi walikuwa wamemzunguka huku waandishi wa habari wakiwahoji mmoja baada ya mwingine. Mtu mmoja alisikika akisema, “Leo asubuhi niliongea nae kwenye simu tukijadiliana mambo ya kibiashara, nashangaa kusikia mwili wake umekutwa kando ya ziwa. Hakika binadamu wengine ni wanyama tu hawana huruma kabisa sasa ona walivyomkatakata mapanga kila mahali pasipo na huruma yoyote.”

 

Pasipo kujali wingi wa watu wale, Abigail alipenyeza mpaka akafika mahali ambapo Jonathan alikuwa amelazwa. Uso kwa uso alikutanisha macho na binti Magreth. Wote wawili wakiwa wenye majonzi makubwa huku macho yao yakiwa mekundu sana kwa sababu ya kulia. “Tena naomba nisikuone ukimgusa Jonathan wewe mwanamke! Kwani wewe ndiyo sababu ya yote haya,” Abigail aliongea kwa sauti ya juu akimwambia Magreth. “Sababu ya yote kiaje? Si tulikuwa wote nyumbani kwake kabla ya kupatwa na hili janga? Jonathan alituaga kuwa anatoka mara moja na wala asingechelewa kurudi? Sasa inakuwaje unasema mimi ndiyo chanzo?” “Naomba tuheshimiane dada tena usinivuruge kabisa,” Magreth alijibu kwa jazba.

 

 

Walizungumza hayo pasipo kujua miongoni mwa wale watu waliokuja kumuona Jonathan hospitalini hapo kulikuwa na askari. “Haya nyinyi nyote mpo chini ya ulinzi naomba tuongozane kituoni bila ubishi!” Mtu mmoja kati ya wale watu ambaye hakuna aliyekuwa akijua kama ni askari, aliwaamuru Abigail na Magreth kuelekea kituo cha polisi. Hakika kubishana kwa hao wawili kuliwaponza na kupelekea kukamatwa kama watuhumiwa namba moja.

 

Wakiwa katika kituo cha polisi, Abigail na Magreth walijaribu kujitetea sana lakini askari hakuwaelewa. Waliwekwa rumande wakingoja uchunguzi uendelee. Abigail alimuomba askari amruhusu apige simu nyumbani kwake ili atoe taarifa ya kuwa amekamatwa. Askari alimruhusu na moja kwa moja alimpigia Felix. “Mume wangu nipo polisi wamenikamata kama mtuhumiwa namba moja wa tukio lililomtokea Jonathan. Naomba uje tafadhali,” Abigail alizungumza huku analia.

 

Felix aliendesha gari lake haraka kuelekea kituoni hapo. Kwa kuwa hata Felix naye alikuwa mmoja wa wafanyabiashara maarufu jijini hapo, maaskari walipomuona walimchangamkia sana. “Vipi bosi mbona usiku usiku umetuletea habari gani?” Aliuliza mmoja wa askari waliokuwa mapokezi. “Mke wangu kanipigia simu anasema mmemkamata kama mtuhumiwa! Kwani vipi mbona kipindi hilo tukio linatokea mimi nilikuwa naye nyumbani?” Alijibu Felix. “Kuna mazungumzo walifanya kati yake na mdada mmoja hivi wakiwa pale hospitalini na mazungumzo hayo yalileta utata kwani wanadai kuwa kabla ya Jonathan kupatwa na hilo tukio alikuwa nao wote nyumbani kwake,” askari alijibu. “Hahahaha…hii habari ndiyo unaniambia wewe mkuu, basi naomba uwaachie wote kwa dhamana huku mkiendelea kufanya uchunguzi wenu mkuu,” Felix alijibu huku anacheka. Abigail na Magreth waliruhusiwa kuondoka usiku uleule kwa dhamana.

 

Heri Niwe Peke Yangu – 03

 

******************ITAENDELEA*********************

Jalia Yusuph
Simu: 0622 216 238
@kalamu_na_karatasi

Toa comment