Jaji Mkuu, George Masaju Awaasa Mawakili Wapya Kudumisha Uadilifu, Utawala Wa Sheria

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, George Masaju amewaasa Mawakili wapya kuwiwa kuona haki ikitendeka, huku wao wakiwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa wanatenda haki kwa wananchi, kuzingatia uadilifu na wakijikita katika sehemu kuu mbili za uadilifu ambazo ni kuzingatia Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Sheria zinazoongoza utumishi na maadili ya mawakili, sambamba na mila na desturi za Tanzania, kudumisha Utawala wa Sheria na kutokuwa chanzo cha uvunjifu wa amani.
Masaju ametoa wito huo Desemba 5, 2025 kwenye Sherehe za Kuwapokea na Kuwakubali Mawakili wapya 774 iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma.

“Sasa mimi nichukue nafasi hii kuwaasa kwamba mtataka na kuendelea kuwa watu wenye akili nzuri, kama Mawakili, moja mtapaswa kuwa ‘sensitive to justice’ muwiwe kuona haki inatendeka na ninyi wenyewe mtende haki, la pili mnapaswa kuwa waadilifu, uadilifu uko kwa maana mbili, moja kuzingatia Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zikiwemo na zile Sheria zinazoongoza utumishi wenu wa uwakili na ni sheria ya mawakili na sheria ya maadili zinazotungwa na hiyo sheria lakini kuzingatia maadili na mila za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Jaji Mkuu.



