Ilipoishia wiki iliyopita
Nilimwacha Michael aondoke lakini ukweli ni kwamba hata mimi mwenyewe nikaanza kumuonea huruma, alikuwa kijana mpole, hakustahili kukaripiwa, alikuja kwangu kwa ajili ya kunijulia hali tu lakini kutokana na hali niliyokuwa nayo, likatokea la kutokea.
Stori za kifo cha Hemedi ziliendelea kusikika shuleni hapo, taarifa zikatapakaa kwamba usiku uliopita aliaga kwamba anakwenda kuonana na msichana maeneo ya Sinza, akaondoka kuelekea huko lakini hakurudi na maiti yake ilikutwa chumbani ikiwa imekakamaa.
Marafiki zake walihuzunika mno, hawakujua ni mwanamke gani aliyekuwa naye ambaye alimsababishia kifo hicho kwani ni mara nyingi sana Hemedi alifanya mambo yake kisiri ili aweze kutembea na wasichana wengi.
Tetesi zile ziliendelea kusikika kwamba kulikuwa na msichana ambaye alikuwa akitembea naye kutoka shuleni hapo, inawezekana ndiye ambaye alisababisha kifo cha Hemedi, marafiki zake wakaanza kuulizana, huyo msichana alikuwa nani? Na si kwao tu, hata wanafunzi walipozipata taarifa hizo nao wakaulizana, huyo msichana alikuwa nani? Kila walipoulizana, hawakupata jibu lolote lile.
******
“Naomba unisamehe Michael.”
“Umenikasirisha sana.”
“Najua, naomba unisamehe.”
“Au kwa sababu ulijua kwamba ninakupenda ndiyo maana ukaamua kunidhalilisha?”
“Hapana! Naomba unisamehe.”
Nilisimama mbele ya Michael, nilikuwa nikimuomba msamaha kwa kile nilichokuwa nimekifanya, nilimdhalilisha, alijisikia aibu na hakukuwa na kitu kingine cha kumwambia zaidi ya kumuomba msamaha.
Moyo wangu ulinihukumu sana, kitendo nilichomfanyia Michael kilikuwa cha aibu sana hivyo nilipaswa kumuomba msamaha. Katika hilo naye akaanza kuunganisha mambo yake, aliniambia wazi kwamba alinisamehe kwa sababu alikuwa akinipenda.
Alionekana kuwa na mapenzi ya dhati kwangu, alionesha kila dalili ambazo mwanaume mwenye mapenzi ya dhati alitakiwa kumuoneshea mwanamke. Niliziona dalili zote hizo lakini pamoja na hayo yote, sikutaka kuwa na mvulana huyo hata mara moja.
Wiki moja ilikuwa imepita tangu Hemedi afariki dunia chumbani, sikutaka kuona mwanaume mwingine akifariki kwa sababu yangu, niliogopa, nilikuwa na moyo wa huruma, sikutaka kumuona Michael akifariki dunia.
“Davina…”
“Abee…”
“Nakupenda sana.”
“Najua.”
“Kwa hiyo?”
“Siwezi kuwa nawe.”
“Kwa nini?”
“Sina sababu! Siwezi tu kuwa nawe.”
“Au hunipendi?”
“Sijui.”
“Hujui nini sasa?”
“Kama nakupenda au sikupendi.”
Sikutaka kumwambia ukweli, kiukweli sikutaka kuwa naye lakini bado nilikuwa na moyo wa huruma juu yake. Nilijua fika kwamba endapo ningemwambia ukweli kwamba simpendi angehuzunika sana, angeumia na hivyo kumuonea huruma kila nitakapokuwa nikimuona.
Michael alining’ang’aniza lakini msimamo wangu ulikuwa uleule kwamba nisingeweza kuwa naye kwa sababu niliamini ilikuwa ni lazima siku moja tufanye mapenzi na baada ya hapo ambacho kingefuatia ni mauti tu.
Itaendelea wiki ijayo.