The House of Favourite Newspapers

JPM: HII NI DHARAU, AAGIZA MSAKO WANAODAIWA BIL. 38 ZA JWTZ – VIDEO

RAIS John Magufuli ametoa muda wa mwezi mmoja kwa taasisi, mashirika, makampuni na watu wote wanaodaiwa jumla ya Tsh. Bilioni 38 na Jeshi la Wananchi (JWTZ) kwa kukopa matrekta ya Suma JKT kwa ajili ya mpango Kilimo Kwanza, kulipa madeni yao mara moja.

 

Maagizo hayo ameyatoa leo alipokuwa akizindua kituo cha uwekezaji cha JWTZ eneo la Mgulani jijini Dar es Salaam  baada ya kuombwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, CDF Jenerali Venance Mabeyo alisaidie jeshi hilo kutilia mkazo  wanaodaiwa warejeshe madeni hayo.

 

Awali Mabeyo alisema taasisi za serikali na watu binafsi walikuwa wanadaiwa Tsh. Bilioni 40 lakini baadhi yao wamelipa Bilioni 2 hivyo zimebaki Bilioni 38 huku Bilioni 3.4 zikidaiwa na Jeshi kwa taasisi za serikali kupitia kampuni ya ulinzi ya Suma Guard.

 

“Kwa wanaodaiwa Shilingi Bilioni 38 na Jeshi kupitia mradi wa matrekta, ninawapa mwezi mmoja walipe, baada ya hapo muanze kuwasaka, haiwezekani mtu anakopa kwa raha hataki kulipa. Kukopa ni harusi kulipa matanga, sasa nataka kukopa iwe harusi na kulipa harusi. Tunatumia gharama kubwa kuanzisha hivi viwanda halafu mwingine hataki kulipa deni.

 

“Nakuomba CDF uwaandikie barua taasisi zote zinazodaiwa na Suma Guard, Tsh. Bilioni 3.4, hata kama inadaiwa Ikulu andika na mimi uniandikie nakala, ili mtakapozifuatilia na zikilipwa na mimi nijue. Haiwezekani mtu anaanza kuchezea hadi jeshi letu. Ndiyo maana hata Mungu anaitwa Mungu wa Majeshi, maana yake Jeshi linatambulika hata kwa Mungu, na linaheshimika,” alisema.

 

Aidha, alimwomba Jen. Mabeyo kumpelekea majina ya wastaafu wa jeshi hilo ili awape nafasi za kazi katika bodi mbalimbali kutokana na kile alichosema hupata shida katika kutafuta na kupata watu wa kuwapa nafasi hizo na kwamba wastaafu wengi wameendelea kuwa waadilifu hata baada ya kustaafu kwao.

 

Pia amesema anatambua uwezo wa Majeshi ya Ulinzi nchini, hasa katika utendaji wa kazi, ujenzi wa Taifa, ulinzi wa mipaka na kuimarisha amani ya nchi  akisema anatamani kungekuwa na timu ya soka ya jeshi ambayo anaamini ingekuwa imechukua hata Kombe la Afrika.

Comments are closed.