visa

Jumanne Mhero Ngoma: Mvumbuzi wa Tanzanite

tanzanittmann_87929

Jumanne Mhero Ngoma

Madini aina ya Tanzanite huiingizia Tanzania kiasi cha dola milioni 20 (zaidi ya Sh bilioni 30) kwa mwaka lakini mgunduzi wa madini hayo, Jumanne Mhero Ngoma, anaishi kwa kutegemea watoto wake, taifa kwa nini halimuoni?

Mzee huyu amefanya mahojiano na vyombo mbalimbali vya habari nasi tumeona leo aingie katika safu hii kama mmoja wa Watanzania walioleta mabadiliko katika sekta ya madini asiyejulikana na wengi.
Katika nchi nyingine zinazothamini watu wake, huyu alitakiwa kufahamika kitaifa au kimataifa. Je aligunduwaje madini ya Tanzanite? Anasema:
“Mara ya kwanza kuyagundua madini haya nilikuwa mdogo sana. Nilikuwa na umri wa chini ya miaka 20 na nilikuwa porini nikichunga mifugo.

“Nilikuwa kwenye msitu ambao Wamasai walikuwa wameupa jina la Lalouo. Eneo ambako niliyaona lilikuwa linafahamika kwa jina la Naisunyai ambako kwa kawaida Wamasai walikuwa wakilitumia kunywesha mifugo yao.
“Siku hiyo niliona vitu vinavyowakawaka. Nikawa najiuliza vitakuwa ni vitu gani? Awali nilidhani pengine ni nyoka au wanyama wa hatari. Nikasogea nikiwa na upinde na mshale wangu tayari kwa lolote.
“Nilipogusa na mti niliokuwa nimeushika, nikashangaa mawe yanayong’aa yakitoka ardhini. Vipande vidogo vidogo vyenye rangi ya bluu. Kwa kweli nilivipenda sana.

“Nilishangaa sana lakini ghafla nikakumbuka kuwa nilikuwa nachunga mifugo. Kumbe ng’ombe na mbuzi niliokuwa nawachunga walikuwa wametawanyika. Nikaacha shughuli hiyo ya kutazama madini na kwenda kuwafuata.
“Kwa bahati nzuri, nilifuatilia njia walizopita hadi nikawapata wote,” anasema.
“Hata hivyo, mwaka 1966 Nilikwenda Morogoro kwenye mafunzo ya madini na hatimaye nikafaulu kwenye mafunzo hayo. Ilipofika Juni sita, mwaka 1966, nikapewa cheti cha utafiti ambacho ninacho hadi leo. Pamoja na mambo mengine, cheti hicho kilikuwa kinakuwezesha kufahamu madini na sifa zake mbalimbali,” anasema.
Ni mafunzo hayo ambayo baada ya kuyamaliza yalimfanya Ngoma aweze kugundua madini hayo ya Tanzanite aliyoyaacha kule Umasaini, Mererani.

Anasema: “Ndipo siku moja nikawachukua ndugu zangu kwenda kwenye ule msitu wa Lalouo ili nikayachunguze tena yale madini. Nakumbuka tulichimba karibu kilo sita za madini hayo. Kuna jiwe moja lilikuwa na ukubwa wa takriban gramu 55 hivi. “Nikalipeleka Moshi kwenye Ofisi ya Mkaguzi wa Madini aliyekuwa akiitwa Bills wakati huo. Mzungu huyo. Akayatazama na akasema hajawahi kuona kitu kama kile. Akahisi yanaweza kuwa Blue Tomaline, lakini tukakubaliana kuwa si yenyewe.

“Mimi nikamuuliza sasa mwenzangu unadhani haya ni madini gani? Unajua Wazungu ni watu wakweli, hawapendi kusema uongo. Akasema kwa kweli hajui, akashauri tupeleke kwenye maabara ya serikali Dodoma.
“Nikampa sampo yote niliyokuwa nayo lakini lile jiwe kubwa zaidi nikabaki nalo. Alipoliona, mke wa bwana Bills akaniomba abaki nalo.Nikakataa.

“Nikamwambia kama nikikupa, nitakuwa nakupa nini?  Maana mumeo ambaye ndiye mtaalamu wa mambo haya ameshindwa kuyajua. Nitabaki na hili kama kumbukumbu yangu.
“Ilipofika Septemba 23 mwaka 1967, ndipo nikapokea barua rasmi kutoka maabara ya Dodoma. Vipimo vikaonesha madini yale yanafahamika kwa jina la Zoisite. Ndiyo maana tunasema madini hayo yaligunduliwa rasmi mwaka huo wa 1967 kwa sababu ndipo cheti kile cha maabara kilipotoka,” anasema.
Jiwe hilo kipenzi la mgunduzi huyu likaja kumpotea katika mazingira ya kutatanisha, aliwapa rafiki zake Wahindi waliokuwa wakiishi Handeni kwa ahadi ya kulirudisha, hawakufanya hivyo.
Baada ya kuibiwa jiwe lake hilo, akili ya Ngoma ilifanya kazi haraka na akaamua kwenda kupata leseni ya umiliki wa eneo ambako aliyapata madini yale.
Akapewa viwanja nane kwenye eneo lile la Lalouo ambako alilipia kiasi cha Sh 15 kwa kila kimoja. Akaweka alama zote muhimu na kuamini kwamba lile ni eneo lake halali kisheria na mara wakati utakapofika, ataanza kuchimba madini hayo.
Itaendelea wiki ijayo.
Toa comment