Kagere atoa tahadhari Simba

MSHAMBULIAJI wa Simba, Meddie Kagere raia wa Rwanda ametoa tahadhari kwa wachezaji wenzake akisema kwamba hawatakiwi kuwachukulia kirahisi wapinzani wao UD do Songo, badala yake wanatakiwa kuongeza nguvu na kupambana kufuata maelekezo ambayo watapewa na kocha wao Patrick Aussems.

 

Kagere ambaye juzi Jumanne alifunga mabao matatu ‘hat trick’ walipocheza mechi ya kirafi ki dhidi ya Power Dynamos ya Zambia katika Tamasha la Simba Day, ataiongoza Simba Jumamosi hii kucheza na UD do Songo katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao utapigwa nchini Msumbiji.

 

Straika huyo Mnyarwanda aliyefunga mabao sita katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita, ameliambia Spoti Xtra, kuwa wanatakiwa kuwa na tahadhari kuelekea katika mchezo huo hasa baada ya kikosi hicho kuongezeka nyota wengine wapya.

“Kitu cha kwanza ni kuwa tumemaliza mechi yetu na Dynamo ambayo imekuwa ya mwisho katika mechi za majaribio na tumeweza kufanya vizuri, sasa tunaenda katika mechi za kimataifa. Kuelekea huko tunatakiwa kuwa makini na kuchukulia kwa uzito mkubwa pambano hilo.

 

“Tunachotakiwa kufanya ni kutimiza kile ambacho tunaambiwa na kocha ili tupate matokeo mazuri, lakini pia tunatakiwa kuwa makini kwa sababu timu kwa sasa ina wachezaji wengi wageni ambao kwa msimu uliopita hawakuwepo hivyo haiwezi kuwa kitu rahisi tu kufanya vizuri kama hatutakuwa na tahadhari,” alisema Kagere.
Toa comment