The House of Favourite Newspapers

KAMA ANAKULIZA KILA SIKU, UNAMNG’ANG’ANIA WA NINI ?

Image result for COUPLES CRYING

TUNAPOKUTANA kama hivi, tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwani wapo ambao muda huu wako kitandani wakisumbuliwa na magonjwa mbalimbali huku wengine wakiwa wameshatangulia mbele za haki.  

 

Ndugu zangu, mapenzi yamekuwa yakiwaliza wengi sana, mimi pia yameshawahi kunitenda lakini ilibaki kuwa siri yangu hadi pale Mungu alipokisikia kilio changu na kunipa faraja. Wengine wanalia wakiwa na sababu za msingi kabisa lakini kinachonisikitisha ni kwamba, wapo wanaotoa machozi yao bila kuwepo sababu za msingi za kufanya hivyo.

 

Kila mmoja tunajua ana moyo wa kupenda na moyo ukishapenda bwana, hauwezi kuambiwa kitu. Ndio maana tunaona baadhi ya watu wanafikia hatua ya kusema kwamba, bila mtu fulani maisha yao hayawezi kuwa yamekamilika. Silikatai hilo kwani ndio uhalisi wa mapenzi ya kweli.

 

Unamkuta msichana ametokea kumpenda mwanaume fulani na anafikia hatua ya kumwambia wazi kwamba, hayuko tayari kumkosa na ikitokea hivyo ni bora afe. Si tatizo mtu kuzianika hisia zake kwa yule aliyetokea kumpenda ila sasa, ni kweli bila huyo uliye naye maisha yako hayawezi kukamilika?

 

Ni wazi kwamba ukikosa furaha katika mapenzi, maisha yako hayawezi kuwa ya furaha. Hii inamaainisha kwamba ukimkosa yule uliyetokea kumpenda ni lazima utayumba, hilo halina ubishi kwani wapo waliodiriki kujiua kwa sababu tu aidha wamekataliwa na wale waliotokea kuwapenda au wameachwa na wapenzi wao. Lakini sasa cha kujiuliza ni kwamba, ni kweli ukiachwa na mpenzi ndio mwisho wa kupendwa? Je ukikataliwa na yule ambaye moyo wako umetokea kumpenda unadhani hutapenda tena?

 

Lahasha! Hizo ni hatua tu miongoni mwa zile za kumpata mtu sahihi katika maisha yako. Kukataliwa na kuachwa na wapenzi kupo katika maisha yetu ya kila siku na ndio maana kila siku wapo wanaoachwa na wanaoingia katika uhusiano mpya. Kwa maana hiyo basi, itakuwa ni umauzi wa busara kumuacha mtu ambaye unahisi hawezi kutimiza ndoto za maisha yako.

 

Hayo ndiyo maisha ya kimapenzi. Ndio maana nasema hata kama umempenda vipi, epukana na mawazo ya kwamba huwezi kuishi bila yeye au maisha yako hayawezi kukamilika bila yeye, yeye ni nani kwani? Kumpenda tu ndio iwe sababu ya yeye kuishika sehemu kubwa ya maisha yako? Hayo ni mawazo potofu kabisa ambayo yanaweza kukufanya ukajikuta uko ndani ya utumwa mwa mapenzi.

Related image

Utalazimika kuingia huko kwa sababu, hata akikutenda huwezi kuwa na ujasiri wa kumuacha, utakuwa tayari akulize kila siku lakini usimkose katika maisha yako. Hivi kutakuwa na maisha ya furaha kweli? Nadhani kikubwa ni kumpenda, kumheshimu na kumthamini ukitarajia hivyo hivyo kutoka kwake.

 

Lakini pia sema na moyo wako na kuutaarifu kabisa kwamba, hutakuwa tayari kuumizwa, utakuwa tayari kumkosa huku ukiamini kwamba, kumkosa yeye haiwezi kuwa mwisho wa maisha yako. Hiyo ndiyo kanuni inayoweza kukusaidia.

 

Epukana na ulimbukeni wa kung’ang’ania penzi linaloumiza kwa sababu tu umeshajijengea katika akili yako kwamba, huyo uliye naye ni mzuri, mtamu kuliko wengine. Yawezekana huyo si uliyepangiwa na Mungu bali yupo mwenye nafasi ya kukupa mapenzi ya kweli yanayoweza kukufanya uhisi umependelewa.

 

Kwa nini nimeamua kuandika makala haya? Nimefanya hivi kutokana na ushauri ambao baadhi ya wasomaji wangu wamekuwa wakiniomba mara kwa mara. Yupo dada mmoja wa Dar ambaye aliomba nisiliandike jina lake gazetini, anasema yeye ana mpenzi wake huu ni mwaka wa pili sasa, anampenda kuliko maelezo.

Image result for COUPLES CRYING

Kumpenda kwake huko imefika wakati hata mwanaume huyo akimkosea badala ya kuombwa msamaha, yeye ndiye anayeomba ili tu wasiachane. Amekuwa akisalitiwa mara kwa mara lakini kila ikitokea hivyo, anamsamehe na kuendelea eti anasema licha ya kutendwa, hayuko tayari kumkosa mwanaume huyo kwani anahisi anaweza kufa! Huyu ni mmoja tu kati ya wengi walio katika mazingira haya, wanalizwa na wapenzi kila wakati lakini kwa sababu tu wanawapenda, wanavumilia ili wasiwakose.

 

Huo ni ulimbukeni kabisa. Mpenzi wako kukutenda ni dalili ya wazi kwamba hana mapenzi ya kweli kwako, ya nini uumie? Huoni kuendelea kumkumbatia ni sawa na kujitafutia vidonda vya tumbo bure? Fanya maamuzi sahihi! Ni hayo tu kwa leo, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine kali!

Comments are closed.