KAZI KWELI KWELI… WANAWAKE WAMTAITI KINYAIYA

MTANGAZAJI maarufu Bongo, Benny Kinyaiya, Ijumaa iliyopita alipata wakati mgumu baada ya kutaitiwa na kundi la wanawake waliokuwa wakimtaka awape msaada. 

 

Tukio hilo lililotokea Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda aliwakutanisha na kuwafuturisha mastaa na watu wasiojiweza wakiwemo walemavu. Ama baada ya futuru kumalizika ndipo wanawake hao walimuona Kinyaiya na kuanza kumtaiti wakimtaka awape pesa.

 

Wanawake hao walianza kumzengea Kinyaiya kama masihara lakini baadaye waliongezeka na hoja yao ikiwa: “Tunaomba msaada.”

 

Awali maombi hayo yalionekana kutomgusa Kinyaiya lakini alipoona wanawake hao wanazidi kuwa ‘siriaz’ kiasi cha kumzonga, aliamua kutoa fungu la fedha ambalo halikujulikana kiasi chake na kuwaambia waende wakagawane. Fungu hilo lilichukuliwa na kundi la kina mama ambao walichukuzana hadi pembeni ambako walikwenda kugawana.

 

Aidha, inaonekana mgao huo haukuzingatia usawa kwani baada ya muda wanawake wengine walimrudia Kinyaiya na kumuambia: “Sisi tumekosa, uliowapa fedha tugawane wametufukuza.”

 

Kwa kuwa wanawake hao walikuwa wakionesha hali ya kusikitika Kinyaiya aliamua kutoa kiasi cha shilingi elfu arobaini na kuwataka nao wakagawane. Hata hivyo awamu hiyo ya mgao haikuwakata kiu baadhi ya wanawake waliokuwepo eneo hilo kwani nao walirudi na kusema hawakunufaika na mgao wa pili kutokana na wagawaji kuwaambia kuwa, hawahusiki.

Kufumba na kufumbua msaada uligeuka kuwa mtiti ambapo kundi kubwa la wanawake liliendelea kumzonga na kumtaka Kinyaiya awasaidie fedha. Mambo yalipomzidi mtangazaji huyo alitaka kuondoka eneo hilo lakini haikuwa rahisi hadi pale baadhi ya wanaume walipojitokeza na kumtoa katikati ya wanawake waliokuwa wamemzonga huku wengine wakimvutavuta.

 

Wakizungumza na paparazi wetu wanawake hao walisema, wameamua kumtaiti mtangazaji huyo awape msaada na si mtu mwingine baada ya kusikia ameoa mwanamke mwenye fedha.

 

“Huyu ana mihela, juzi tu tumesikia amemuoa mwanamke tajiri aliyekuwa akiishi Ulaya,” alisema mwanamke mmoja ambaye jina lake halikufahamika. Alipoulizwa Kinyaiya kuhusiana na tukio hilo mtangazaji huyo alisema: “Hakuna tukio baya; sema ndiyo hali zetu, wewe mwenyewe unajua.


Loading...

Toa comment