The House of Favourite Newspapers

KESI YA VIGOGOGO NANE WA CHADEMA KUUNGURUMA JULAI 2

MAHAKAMA  ya Hakimu Mkazi Kisutu, inatarajia kutoa uamuzi wa muda wa kusitisha ama kutositisha usikilizaji wa kesi inayowakabili viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwemo mwenyekiti wake Freeman Mbowe Julai pili mwaka huu.

 

 

Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa mashtaka kupinga maombi yaliyowasilishwa na upande wa utetezi.

 

Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi amewasilisha maombi hati kinzani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbrad Mashauri ambapo amepinga usitishwaji wa kesi hiyo kwa sababu maombi yao ni batili.

 

Wakili huyo  amedai msingi mkuu wa pingamizi hizo ni kwamba maombi ya waombaji ni batili kwa kuwa utaratibu uliotumika kuielekeza mahakama hiyo iweze kutoa amri walizoomba una dosari.

 

Alidai kwamba  mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo na kutoa nafuu zilizoombwa, hivyo aliomba yatupiliwe mbali.

 

Upande wa utetezi maombi yaliwasilishwa  na Peter Kibatala ambaye ameiomba mahakama isimamishe kwa muda usikilizwaji wa kesi hiyo kwa sababu wamewasilisha maombi ya marejeo Mahakama Kuu ya Tanzania juu ya uamuzi mdogo uliotolewa na mahakama hiyo.

 

Kutokana na mvutano wa kisheria, Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi Julai pili mwaka huu.

 

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.

 

Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na Mbunge wa Tarime mjini, Esther Matiko.

 

Inadaiwa kuwa washtakiwa walitenda makosa hayo Februari 16, mwaka huu katika maeneo ya Viwanja vya Buibui, Mwananyamala na barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni.

 

 

Comments are closed.