The House of Favourite Newspapers

Kigwangalla: Fedha za Mlima Kilimanjaro Kutokomeza UKIMWI

Waziri wa Maliasili na Utalii. Dk. Hamis Kigwangalla (wa pili kushoto) akiwa  na baadhi ya viongozi na washiriki wa kampeni ya kupanda mlima Kilimanjaro kwa lengo la kukusanya fedha za kutomomeza VVU nchini. Kampeni hiyo iliyodumu kwa miaka 17 sasa imeratibiwa na Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM) na Tume ye Kudhibiti Ukimwi nchini (TACAIDS).

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dk. Khamis Kigwangala amesema anatarajia kuandaa utaratibu wa makundi ya watu mbalimbali wakiwamo viongozi mashuhuri na wasanii kupanda Mlima Kilimanjaro ili kuchangisha fedha za kuendeleza mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi.

Kigwangala ametoa kauli hivi karibuni mkoani Kilimanjaro wakati akizindua zoezi la upandaji Mlima Kilimanjaro lililoshirikisha zaidi ya watu 80 kutoka nchi mbalimbali kwa lengo la kuchangisha fedha za mapambano dhidi ya Ukimwi kupitia kampeni ya ‘Geita Gold Mining Kilimanjaro Challenge 2019’.

 

Kampeni hiyo  iliyoratibiwa na GGM kwa kushirikiana na TACAIDS  pia imelenga kutunisha mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF).

 

Alisema wizara ya maliasili na utalii itaandaa utaratibu wa kuhamasisha makundi ya watu mbalimbali wakiwemo wasanii na watu mashuhuri duniani kupanda Mlima Kilimanjaro ili kuchangisha fedha za mapambano dhidi ya Ukimwi kwani mapambano ya virusi hivyo ni ya watu wote na si ya serikali pekee.

 

“Takwimu za maambukizi mapya hususan katika kundi la vijana yanatisha na kwamba zinahitajika jitihada za makusudi kutoka katika kundi hilo kudhibiti ugonjwa huo.

Dk. Kigwangalla (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa GGM, Richard Jordinson. wakati wa  uzinduzi wa zoezi la kupanda Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kukusanya fedha za kutokomeza maambukizi ya VVU nchini.    Zaidi wa wapandaji 80 wameshiriki kampeni hiyo.

“Hali ya maambukizi mapya ya VVU inatisha, ni lazima sisi kama vijana  tuwe msitari wa mbele kupambana na hali hii, nimepanga kupanda mlima huu na watu mashuhuri wakiwemo wanasiasa na wasanii ili kuchangisha fedha kwa ajili ya kudhibiti ugonjwa huu.

 

“Lakini pia nimefurahi kuona kuwa miongoni mwa wanufaika wa kampeni hii ni wapagazi takribani 150 waliopatiwa mafunzo ya kujilinda na VVU na masuala mbalimbali kuhusu udhibiti wa Ukimwi. Kundi hilo pia limepatiwa mafunzo ya ujasiriamali kwa lengo la kuwasaidia wawe na kipato endelevu,” alisema. 

 

Aidha, Mkurugenzi wa TACAIDS, Dk. Leonard Maboko, alisema kila siku watu zaidi ya 200 huambukizwa VVU ambapo kati yao asilimia 80 ni vijana kwanzia miaka 15-24.

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa GGM,  Richard Jordinson, amesema kampeni hiyo imewezesha ukusanyaji wa zaidi ya Sh bilioni 13 tangu ilipoanzishwa miaka 17 iliyopita.

Baadhi ya washiriki wa kampeni ya kupanda Mlima Kilimanjaro ‘Kili challenge 2019’ inayoratibiwa na GGM na TACAIDS.

Alisema katika kampeni ya mwaka huu zaidi ya watu 80 wameshiriki ambapo kati yao 32 watapanda mlima, 28 watauzunguka kwa kutumia baiskeli na watu 17 kutoka nchi mbalimbali wameshiriki kampeni hiyo ya kupanda mlima Kilimanjaro.

 

“Upandaji huo utachukua siku saba ambapo wameanza kupanda  Juni 15 na watashuka Juni 22 mwaka huu,” alisema.

 

Aliongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa kampeni hiyo miaka 17 iliyopita zaidi ya taasisi binafsi na mashirika 50 yanayotoa misaada na elimu ya Ukimwi nchini yamenufaika na kampeni hiyo.

NA MWANDISHI WETU

Comments are closed.