The House of Favourite Newspapers

Kimenuka! Fumanizi la Mwezi Mtukufu Laibua Ndoa Mpya!

Mke wa Sele Gogo, Shani ldd (mwenye dela lenye rangi nyekundu na nyeupe) akiwa na kundi lake nje ya chumba cha Mwajabu,

 

KUNA mambo ya ajabu ya kila aina ambayo hutokea kwa nyakati tofauti, lakini hili lililojiri katika kipindi hiki cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, ni kali zaidi.

Mke wa mfanyabiashara maarufu wa unga wa sembe mjini hapa, Seleman Husein almaarufu Sele Gogo aliyefahamika kwa jina la Shani Idd, anadaiwa kuzua timbwili zito katika tukio la fumanizi.

 

Timbwili hilo la fumanizi linatajwa kutibua ndoa ya wawili hao kisha kuibua ndoa mpya kati ya Sele Gogo na mwanamke aliyedaiwa kufumwa naye, Mwajabu Juma ambaye baada ya kizaazaa hicho aliamua kufunga naye pingu za maisha.

Kwa mujibu wa mashuhuda, fumanizi hilo lililojaza umati lilijiri kwenye chumba cha Mwajabu kilichopo Mtaa wa Makaburi B Kata ya Mji Mpya mjini hapa wakati wa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

 

Sele Gogo na Mwajabu wakiwa kwenye pozi baada ya kufunga ndoa,

Mashuhuda hao walidai kwamba, baada ya majirani kumshuhudia Sele Gogo ambaye pia ni msagishaji wa unga akizama mara kwa mara kwenye chumba cha Mwajabu, waliamua kumtonya mke wa jamaa huyo.

 

Ilidaiwa kwamba, baada ya kulambishwa ubuyu huo, Shani, bila kuchelewa, aliwataarifu mashosti zake zaidi ya sita kisha walishonesha sare za madera kwa ajili ya shughuli maalum.

Baadaye ilielezwa kuwa, Shani aliwaweka wazi wenzake kwamba sare hizo zilikuwa ni kwa ajili ya shughuli ya fumanizi na kweli ilipofika siku ya tukio, aliwatonya, kisha wakatinga mtaani hapo.

Kuna madai kwamba, walipofika kwenye chumba cha Mwajabu, Sele Gogo alikuwepo ndani hivyo wakaamsha popo ile mbaya kiasi cha kufunga mtaa kwa vurugu.

 

Ilisemekana kwamba, baada ya zogo kushika kasi, baadhi ya mashuhuda waliamua kumtonya mwandishi wetu ambaye alifika fasta na kushuhudia varangati hilo likiendelea.

Kwa mujibu wa mashuhuda hao, Sele Gogo, baada ya kuona hali ya hewa imechafuka, alikurupuka ndani na kutimka zake huku akiwaacha wanawake hao wakipambana na Mwajabu kabla ya kumtia mikononi na kuzichapa naye kavukavu.

 

 

 

Kufuatia hali hiyo, mwanahabari wetu aliamua kwenda kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo, Amani Kombo ambaye baada ya kusimuliwa kisa na mkasa juu ya fumanizi hilo alisema hawezi kwenda eneo la tukio kwa kuwa alikuwa anaumwa.

 

 

Katika hali kama hiyo, ilibidi mwandishi wetu awaite polisi ambao walifika na difenda na kuwachukua Shani na Mwajabu.

 

Taarifa zilizopatikana ndani ya Jeshi la Polisi zilieleza kwamba, wahusika hao walipofikishwa polisi, waliamuriwa wampigie simu Sele Gogo ambaye alifika kituoni hapo na alipoulizwa juu ya sakata hilo alidai Mwajabu ni mchumba’ke anayetaka kumuoa kama dini yake ya Kiislam inavyomruhusu kuoa wake zaidi ya mmoja huku akimshutumu Shani kumfumania na kumjazia watu.

 

Ilielezwa kuwa, baada ya Sele Gogo kuyasema hayo, polisi walimuamuru kuwachukua wake zake na kuondoka nao ambapo alimkana Shani na kuamua kuondoka na Mwajabu.

Siku iliyofuata baada ya tukio hilo, gazeti hili lilizungumza na Sele Gogo juu ya tukio hilo ambapo alikiri kutokea kwa fumanizi hilo alilodai lilikuwa la kupanga. “Huyu Mwajabu ni mchumba wangu wa muda mrefu. Wambeya walimwambia mke wangu, akaja na kundi lake kunifumania.

 

Shani mke mkubwba wa Sele.

“Kwa hasira nimeamua kumuoa kabisa Mwajabu kukata mzizi wa fitina,” alisema Sele Gogo ambaye kweli siku mbili baadaye alifunga ndoa na Mwajabu. Kwa upande wake Shani alikuwa na haya ya kusema: “Mimi na mume wangu tumefunga ndoa miaka 11 iliyopita. Tumejaliwa watoto wawili na mali kadhaa ikiwemo nyumba tunayoishi Mji Mwema, Nane-Nane na tuna viwanja kadhaa.

 

“Hajawahi kuniambia kama ana mchumba au anataka kuoa hadi wasamaria wema waliponitonya kuwa kila siku mume wangu anaingia chumbani kwa Mwajabu. “Kweli nilifika kwenye chumba hicho na kumkuta mume wangu ndani. Baada ya mume wangu kuniona alifungua mlango akatoka nduki na kuniachia huyo mwanamke akataka kunikata na kioo.

 

“Nakushukuru mwandishi kwa kuita polisi maana hali ingekuwa mbaya. “Simtaki tena Sele Gogo, nimeamua kwenda Bakwata (Baraza la Waislam Tanzania), baadaye ninakwenda mahakamani kudai talaka yangu tugawane mali, kila mtu aendelee na maisha yake binafsi, ukewenza siuwezi.”

STORI: Dunstan Shekidele, Morogoro

Comments are closed.