Kiongozi Mkuu wa Iran Amtabiria Trump Anguko, Amlinganisha na Farao

Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ametoa onyo kali kwa viongozi wa kimataifa wanaotumia nguvu zao vibaya, akitabiri kuwa Rais wa Marekani Donald Trump atakumbwa na anguko kama la watawala dhalimu wa kihistoria.
Kupitia machapisho yake mbalimbali katika mtandao wa X siku ya Ijumaa, Khamenei ametumia mifano ya kidini na kihistoria akisema: “Rais wa Marekani anayehukumu dunia nzima kwa kiburi anapaswa kujua kuwa madikteta na watawala wenye kiburi duniani, kama vile Farao, Nimrodi, Mohammad Reza [Pahlavi] na wengineo, walishuhudia anguko lao walipokuwa kwenye kilele cha majivuno yao. Yeye pia ataanguka.”
Khamenei ameendelea kuishutumu Marekani kwa kile alichokiita “uongozi wa kitapeli,” akitolea mfano uingiliaji wa Marekani katika mataifa ya Amerika ya Kusini hasa Venezuela. Ameeleza kuwa Marekani haina hata aibu kukiri maslahi yake ya kiuchumi:
“Unaweza kuona jinsi walivyoizingira nchi moja kule Amerika ya Kusini na kuchukua hatua fulani huko. Hawana hata aibu na wanasema waziwazi kuwa walifanya hivyo kwa ajili ya mafuta. Kwa ajili ya mafuta! Wanasema wamefanya hivi kwa ajili ya mafuta.”
Huku mvutano ukizidi kufuatia uamuzi wa Trump wa kuwaunga mkono waandamanaji nchini Iran, Khamenei amesisitiza kuwa Washington inaendelea kufeli kutokana na kutokuijua vyema jamii ya Iran:
“Maadui zetu hawaifahamu Iran. Huko nyuma, Marekani ilishindwa kutokana na mipango yao mibovu. Leo pia, njama zao mbovu zitawafanya washindwe. Leo kama ilivyokuwa zamani, Marekani imekosea katika mahesabu yake kuhusu Iran.”

