The House of Favourite Newspapers

Kocha Mkuu wa Simba Atembea Na Faili La Usajili Msimu Ujao

0
Kocha Mkuu wa Simba, Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’.

UONGOZI wa Simba, umeibuka na kutamba kuwa, tayari Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ tayari ana majina ya wachezaji wanaotakiwa kusajiliwa kwa ajili ya msimu ujao.

Simba imepanga kukifanyia maboresho kikosi chao kuelekea usajili ujao wa dirisha kubwa ili kuhakikisha wanafanya vema tofauti na walivyofeli msimu huu.

Tetesi zilizokuwepo hivi sasa, Simba imepanga kusajili wachezaji nane pekee, kati ya hao wapo wa kigeni na wazawa wenye uwezo na uzoefu wa kucheza michuano ya kimataifa.

Wapo baadhi ya wachezaji wanaotajwa kuhitajika na Simba msimu ujao, ambao ni beki wa kati wa Rayon Sports ya Rwanda, Abdul Rwatubyaye na kipa wa Vipers ya Uganda, Alfred Muderekeza.

Wengine ni kiungo mshambuliaji wa RS Berkane ya Morocco, Victorien Adebayor na kiungo wa Geita Gold, Edmund John.

Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema kocha huyo tayari ana majina hayo ambayo amepanga kuyakabidhi mara baada ya michezo ya Ligi Kuu Bara kumalizika.

Ally alisema mara baada ya mchezo wa mwisho wa ligi kuchezwa Juni 9, mwaka huu, haraka Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba watakutana na Kocha Robertinho kwa ajili ya kuyapitia majina hayo.

Aliongeza kuwa, baada ya hapo haraka uongozi utaanza kazi yake ya kukamilisha usajili huo wa wachezaji ambao wamependekezwa kwa ajili ya kusajiliwa.

“Kilichobaki hivi sasa katika usajili wetu mpya ni utekelezaji wa kuwapa mikataba wachezaji wapya tuliokuwa katika mipango ya kuwasajili msimu ujao.

“Kocha tayari ana majina yake ya wachezaji ambao amewapendekeza, licha ya kuwepo baadhi anaendelea kuwafuatilia kwa karibu kujua viwango vyao,” alisema Ally.

STORI NA WILBERT MOLANDI

Leave A Reply