Kuchelewa Kuzaa Kunavyosababisha Uvimbe Kwenye Kizazi
UVIMBE kwenye kizazi kitaalamu huitwa fibroids na hauhusiani na kansa, hushambulia mji wa mimba na kusababisha usumbufu mkubwa kwa akina mama ambao huweza kuwaleta tatizo wakati wa hedhi kwa kusababisha kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi.
Pia husababisha mwanamke kuwa na maumivu makali wakati wa hedhi na huweza kusababisha mwanamke akashindwa kubeba mimba au kama kama atabahatika kupata mimba, basi huishia kuharibika hivyo kuleta mushkeli katika ndoa au mahusiano na hii huwatokea zaidi wanawake ambao huchelewa kuzaa.
Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 20 ya wanawake wote wenye umri wa miaka kati ya 30 na kuendelea, hasa ambao hawajahi kuzaa au waliokaa muda mrefu bila kunasa ujauzito, huwa na uvimbe kwenye kizazi.
Bahati mbaya sana kati ya asilimia 50 huwa na uvimbe bila kuwa na dalili yoyote na takwimu zinaonesha kuwa kati ya asilimia tatu hadi 10 ya wagonjwa wote wanawake wanaohudhuria hospitali za akina mama huwa wanasumbuliwa na uvimbe kwenye kizazi.
Sababu kubwa inayosababisha uvimbe kwenye kizazi haijulikani chanzo chake isipokuwa inasadikika kuwa kuna vitu vichache vinavyochochea mwanamke kuweza kupata uvimbe kwenye kizazi.
Vitu hivyo ni kama hitilafu za kuunganika kwa chembechembe wakati wa mimba kutungwa, kitaalamu hujulikana kama chromosomal abnormality, hii hutokea kwa zaidi ya asilimia 40 kuweza kusababisha uvimbe kwenye kizazi.
Sababu nyingine ni ukuaji usiokuwa wa kawaida wa chembechembe ndogo za mwili zijulikanazo kama polygrowth factor ambazo ni kama zile za sukari zijulikanazo kama insulin.
Sababu nyingine ya kuwepo kwa tatizo hili la uvimbe kwenye kizazi ni urithi ambapo mtu huweza kurithi kutoka kwa ndugu wa karibu kama mama, shangazi, mama mdogo au mkubwa au bibi.
Uvimbe kwenye kizazi huambatana na ukuaji wa vichocheo vya mwili kwa mwanamke vijulikanavyo kama oestrogen, hivyo basi uvimbe hutokea baada ya mwanamke kuvunja ungo kwa kuwa kabla ya kuvunja ungo hawezi kupata uvimbe kwa kuwa vichocheo vya oestrogen vinakuwa bado havijazalishwa.
Uvimbe huweza kuongezeka kipindi cha ujauzito kwa kuwa oestrogen huzalishwa kwa wingi na pia uvimbe huweza kusinyaa baada ya mwanamke kufunga kuingia kwenye hedhi baada ya kuzeeka yaani menopause na hii hutokana na mwili kusimama kuzalisha oestrogen.
VISABABISHI VYA TATIZO
Vitu vinavyochangia uvimbe kwenye kizazi ni kama vile mwanamke kutozaa wakati yupo kwenye umri wa kuzaa, sababu nyingine kubwa ni mwanamke kuongezeka uzito, kitaalamu huitwa obesity.
Pia sababu nyingine ni zile zinazosababisha kuzalishwa kwa chembechembe za vichocheo vya mwili zinazozalishwa mwilini zinazojulikana kama Hyperoestrogen state ambapo vitu vinavyochochea oestrogen iwe nyingi mwilini kama vile dawa za uzazi wa mpango pia dawa zinazosababisha mayai kupevuka kwa wale wenye tatizo la kupata watoto.
Pia uchunguzi unaonesha kuwa watu wenye rangi nyeusi hasa wanawake Waafrika wapo kwenye hatari ya kupata uvimbe kwenye kizazi. Wanawake wanaovuta sigara pia wapo kwenye hatari ya kupata maradhi haya.
AINA MBILI ZA UVIMBE
Kuna aina mbili za uvimbe kwenye kizazi unaoweza kutokea, moja huweza kutokea kwenye mlango wa kizazi na kitaalamu hujulikana kama Cervix na pili sehemu ya ndani ya mfuko wa kizazi ujulikanao kama body of uterus.
Sehemu hii ya ndani nayo imegawanyika kutokana na tando za ukuta wa mji wa mimba, kitaalamu huitwa layer of uterus ambapo hushika asilimia kama 75 ya vile vivimbe vyote na mgonjwa akawa na tatizo bila kuonesha dalili zozote.
Itaendelea wiki ijayo.
Comments are closed.