KWA MPENZI ULIYENAYE UMEPATA , UMEPATIKANA?

MAPENZI huweza kumfanya mtu akaishi maisha ya raha mustarehe hasa pale anapompata mtu mwenye penzi la kweli lakini pia usipoyajulia mapenzi yanaweza kukutoa roho.  Wangapi leo hii wamechanganyikiwa kutokana na kukataliwa penzi na watu waliotokea kuwapenda? Wangapi wamejiua baada ya kuachwa na wapenzi wao? Wangapi wanashindwa kufanya kazi zao kwa ufasaha kwa sababu wamekorofishwa na wapenzi wao?

Hakika ni wengi na kwa maana hiyo basi kama unataka kuishi maisha ya raha, pamoja na mambo mengine hakikisha huchezi kamari kwenye mapenzi, ingia katika uhusiano unaofaa ili mwisho wa siku furaha ichukue nafasi katika kila siku iendayo kwa Mungu.

Wiki hii naomba nizungumzie swali ambalo wengi wamekuwa wakijiuliza bila kupata majibu sahihi kiasi cha kuwafanya washindwe kuishi maisha ya furaha na wapenzi wao. ‘Nimepata au nimepatikana?’ Hili ni swali wanalojiuliza wengi walio katika uhusiano.

Huenda hata wewe ulishawahi kujiuliza swali hili na mpaka sasa hujabaini ukweli wa penzi lake kwako na kama hujawahi kujiuliza swali hili basi hauko makini katika uhusiano wako. Hivi wewe ambaye unajiamini kwamba umepata mtu ambaye anakupenda wa dhati una kipi cha kushika? Unajiridhishaje katika hilo?

Labda niseme tu kwamba, mapenzi ya sasa yamejaa ulaghai wa kupitiliza. Unaweza ukajikuta uko na mpenzi ambaye anaonesha kukupenda sana kiasi cha kukufanya uamini kwamba umepata mtu sahihi lakini kumbe anajifanyisha.

Yaani huo ndio ukweli wenyewe na usishangae hata huyo uliyenaye akawa anakupotezea muda wako tu. Unachotakiwa kukifanya ni kumfanyia uchunguzi wa kina kubaini ukweli wa penzi lake kwako. Niseme tu kwamba, hakuna mtu anayeweza kuwa na uhakika wa asilimia mia moja kuwa mpenzi aliyenaye amepata mtu kwa maana ya mtu kwelikweli na kama unaamini hivyo, unaifurahisha tu nafsi yako kwa kuwa ukweli unaweza usiwe huo.

Huyo uliye naye ndiye mwenye siri moyoni mwake na ndio maana unaweza kukuta mpenzi wako anakusisitizia kwamba anakupenda lakini bado unashindwa kuamini. Wataalam wa masuala ya mapenzi wanasema, kumdhihirishia mpenzi wako kwamba unampenda sio lazima umwambie NAKUPENDA! Vitendo vyako ndivyo vitamfanya aamini hivyo.

Hata hivyo hukatazwi kumpenda mtu lakini bahati mbaya inakuwa pale utakapotokea kumpenda mtu asiyekupenda na ukalazimisha akupende ili kujiridhisha.

Walio katika aina hii ya mapenzi wako wengi. Mtu anaona kabisa mwanaume hamuoneshi kumpenda kwa dhati, hamjali lakini mwanamke anamng’ang’ania tu eti kwa sababu anampenda. Hivi mwanamke kama huyu anashindwa kubaini kuwa mwanaume aliyenaye hana penzi la dhati kwake?

Ifike wakati basi ukae chini na utafakari penzi analokupa mpenzi wako na kuchukua uamuzi sahihi, kumuacha au kuendelea naye. Usikubali hata siku moja kupotezewa wakati na mtu asiyelithamini penzi lako. Ni wakati muafaka wa wewe kujiuliza kama umepata au umepatikana, na kama umepatikana, jinasue lakini kama umepata basi tulia na uyafurahie maisha yako.

 


Loading...

Toa comment