Lady Jaydee Atangaza Kuzindua kitabu chake kipya Juni 9

Msanii mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva, Judith Wambura maarufu kama Lady Jaydee, ametangaza uzinduzi wa kitabu chake kipya ambacho ni wasifu wa maisha yake (autobiography). Kitabu hicho kitaleta simulizi ya safari yake ya miaka 25 katika muziki, ikielezea alipotoka, alichopitia, changamoto alizokutana nazo, mafanikio aliyoyapata na mafunzo aliyojifunza kupitia safari hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Lady Jaydee ameandika, “Nitakuwa na launch ya kitabu/autobiography kuhusiana na safari yangu ya miaka 25. Nilipotoka, niliyoyaona, niliyoyapitia, niliyojifunza, nilipokwama na nilipofanikiwa.”
Uzinduzi wa kitabu hicho unatarajiwa kufanyika ndani ya wiki ya Silver Concert, ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya mafanikio yake katika muziki. Wiki hiyo maalum itaanza tarehe 9 Juni hadi 13 Juni, 2025, ikiwa na shughuli mbalimbali za kusherehekea mafanikio yake kama msanii wa muziki wa Bongo Fleva.