Ligi ya Wanawake inahitaji maboresho zaidi

TUMESHUHUDIA ushindani mkubwa msimu huu kwenye Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania ambayo inadhaminiwa na Bia ya Serengeti Lite ambapo timu zote zilikuwa zikipambana.

 

Kwa sasa timu zote zimebakiwa na mchezo mmoja mkononi ili kukamilisha mzunguko wa pili na kuhitimisha rasmi msimu huu ambapo bingwa wake tayari ni JKT Queens. Wanastahili pongezi.

 

Kwa sasa timu nyingi zitakuwa zimeshajua wapi zilikwama na sababu iliyowafanya wakaboronga kwenye ligi hasa kwa kupata matokeo mabovu kwenye michezo yao waliyocheza.

Tumeshuhudia namna JKT Queens walivyokuwa wakigawa vipigo kwa timu zote ambazo imecheza nazo, hilo lichukuliwe kama funzo kwa timu zote zilizoshindwa kupata matokeo.

 

Hapa timu nyingi zimeshindwa kufurukuta kutokana na aina ya wachezaji waliokuwa wakipigania timu pamoja na benchi la ufundi kwa jumla. Kwa muda huu ambapo ligi inakamilika makosa yote yafanyiwe kazi ili kuboresha vikosi kwa ajili ya msimu ujao maana tayari msimu huu hesabu zimefungwa.

Viongozi wa timu zote waache suala la usajili mezani kwa benchi la ufundi, wasianze kuchanganya majalada, haitakuwa sawa kuelekea kuiandaa timu yenye ushindani. Timu bora inaandaliwa na benchi la ufundi ambalo limeshajua uhitaji wa timu na mapungufu ya timu yalipojificha kwa ajili ya msimu ujao.

 

Tumeona timu ambazo zilikuwa na usajili mzuri namna zilivyokuwa zikipata matokeo chanya muda mwingi licha ya ushindani kuwa mkubwa siku zote.

 

Mfano Simba Queens na Alliance Girls, hawa walikuwa washindani kutokana na aina ya timu waliyokuwa nayo pamoja na usajili bora walioufanya msimu huu bila kuwasahau mabingwa, JKT Queens.

Ni wakati sahihi wa kujipanga upya kwa ajili ya msimu mwingine maana huu wa sasa umeshakamilika, mipango ya mbele inabidi ipigiwe hesabu kali. Tumeona pia timu ambazo hazijafanya vizuri msimu huu zimeishia kupokea zigo la mabao, zipo zilizopigwa mpaka mabao 10, hilo lisiwakatishe tamaa, uwezo bado mnao.

 

Pia kuna sababu ambazo zimekuwa zikichangia kwa timu kuboronga mbali na usajili, hivyo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linapaswa liangalie namna ya kuboresha ligi hii msimu ujao. Kwa mfano suala la usafiri na muda wa kufika kituo cha mchezo, nilifuatilia nikagundua kwamba timu nyingi zimekuwa hazipati muda wa kupumzika kabla ya mchezo kutokana na kuunganisha michezo pamoja na safari.

 

Yaani kuna timu inafika siku ya mchezo na kuunganisha moja kwa moja uwanjani, kwa mtindo kama huu kupigwa ni lazima maana wachezaji wanakuwa wamechoka na uchovu. Ninaamini endapo watapewa muda wa kupumzika na kujiandaa itaongeza ari ya kupambana na ligi itakuwa na msisimko mpya na wenye kuleta raha.

 

Kwa upande wa viwanja, wengi wanacheza kwenye viwanja vilivyo chini ya viwango, hii inachangia kuwavunja moyo wachezaji kuendelea kupambana kwenye mazingira magumu, linapaswa lifanyiwe kazi.

 

Mfano mdogo ni Uwanja wa Karume uliopo katika Makao Makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ukilitazama kapeti utapata picha kwamba wanaotumia uwanja huo wapo kwenye mazingira ya namna gani. Muda wa kulitumia umekwisha na kilichobaki ni kipande tu ambacho hakina ubora ule unaostahili kwa wachezaji kuutumia uwanja huo, ni wakati wa kuboresha.

Kama hicho kipo makao makuu kina hali ya namna hiyo, je vile ambayo vipo nje huko hali itakuaje? Tusimamie na tuboreshe mazingira ya kazi kwa timu zetu. Imani yangu ni kwamba tukiamua na kujipanga vema kila kitu kinawezekana na tutapata maendeleo tunayohitaji.

 

Endapo tutaboresha Ligi ya Wanawake Tanzania tutakuwa na mkusanyiko wa vipaji vingi vitakavotengeneza timu ya taifa bora na yenye kuleta ushindani kimataifa. Hii itasaidia taifa kuepuka aibu ya kuishia njiani kwenye michuano ya kimataifa, tumechoka kuwa wasindikizaji ilihali nguvu kazi tunayo.

MAKALA NA MOHAMMED HUSSEIN


Loading...

Toa comment