The House of Favourite Newspapers

Madhara ya Ulevi na Athari Zake Kiafya-2

0

Tunaendelea kuchambua madhara ya ulevi baada ya wiki iliyopita kusimulia mengi, ni vema kufuata ushauri wa kitaalamu kuhusu utumiaji wa pombe au kilevi aina yoyote kwani kuna faida na madhara kama tutakavyoendelea kuona hapa leo; endelea:

UTUMIAJI ulevi unasababishwa na sababu mbalimbali ambapo mojawapo tunaweza kuashiria masuala ya hali ya wasiwasi, fadhaa, msononeko na kutojiamini au jitihada za kukimbia hali ya fadhaa na kuchanganyikiwa kiakili kwa kiwango fulani.

Baadhi ya watu wakati wanapokuwa na hali ya wasiwasi wakiwa na lengo la kutafuta hali ya utulivu huamua kunywa pombe au kutumia ulevi wakijidanganya kwamba, wakiwa wamelewa wanaweza kuweka hali ya mawazo, msononeko na kujiinamia wanayokabiliwa nayo.

Ukweli wa mambo ni kuwa, katika hatua ya awali, mlevi hupata hisia ya uongo, lakini baada ya muda, athari mbaya za kutumia pombe huanza kudhihirika.

Miongoni mwa athari za wazi kabisa za mtu aliyetumia kileo ni kuyumba, kushindwa kuchukua maamuzi na kuzungumza maneno yasiyo na maana.

Wanawake huathirika zaidi na athari mbaya za pombe ikilinganishwa na wanaume. Maafa yaliyoathiri jamii za kibinadamu kwa kutokana na utumiaji wa ulevi ni makubwa kuliko hata majeraha yanayotokana na magonjwa hatari.

MAGONJWA:

Utumiaji wa ulevi huleta magonjwa mabaya ya kansa ya tumbo na maini, magonjwa ya tumbo, kifua kikuu, magonjwa ya akili kama vile ukichaa na kadhalika na kuharibu vizazi kwa kuathiri viungo kuanzia tumboni na mamilioni ya maovu yanayotokana na ulevi.

Kwa hakika pombe ni sawa na sumu na hivyo hakuna mtu yeyote atakayesema kuwa sumu kwa kiwango kidogo haidhuru ndiyo maana sisi wataalamu wa tiba tunatilia mkazo juu ya suala hili na kusisitiza kuepukana na matumizi ya ulevi ambayo yamesababisha familia nyingi kusambaratika. Hatari nyingine inayowakumba walevi ni akili na seli za fahamu zao huharibiwa vibaya na huweza kupatwa na magonjwa ya kila aina.

Ulevi ni aina mojawapo na mihadarati inayodhuru mishipa ya fahamu. Inadhuru seli za ubongo na kusababisha ukichaa na hata mtu kuwehuka na huharibu ufahamu na busara za mwanadamu na huondoa wema na heshima.

Hivi karibuni Taasisi ya Juu ya Afya nchini Italia ilitangaza kuwa, kila mwaka watu 25,000 huwa waathirika wa utumiaji ulevi. Watu 14,000 kati yao ni wanaume na idadi iliyobakia ni wanawake.

Kiafya walevi wengi hupoteza maisha yao kutokana na figo kutofanya kazi au ajali za barabarani ambazo chanzo chake ni kulewa. Takwimu hizo zinaonyesha kuwa, mabinti na vijana wadogo laki saba wa Kiitalia wanatumia ulevi, suala ambalo limesababisha taasisi mbalimbali za kijamii nchini humo kuonyesha wasi wasi wake juu ya mustakabali wa baadaye wa jamii, hasa kwa kuzingatia kuwa vijana ndiyo taifa la leo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakisia kwamba, gharama za kimatibabu na kijamii zinazotokana na utumiaji ulevi huko barani Ulaya zinafikia Yuro bilioni 125 kwa mwaka. Matumizi ya ulevi huwa na taathira kwa mtu kama vile mto uliofurika kwani, utumiaji ulevi huondoa akili na busara.

Pindi mtu anapolewa na akili kutofanya kazi yake kama kawaida na hivyo kutokuwa na udhibiti wa matendo na maneno yake. Nusu ya matukio ya ukichaa na kuwehuka sambamba na yale matatizo ya kisaikolojia yanatokana na utumiaji ulevi.

Kama tulivyosema hapo juu, ulevi humfanya mlevi kuondokewa na akili na hivyo humfanya afanye mambo ambayo ni kinyume na maadili mambo ambayo akiwa hajalewa hawezi kuyafanya.

Kuna jumla ya magonjwa 60 yanayosababishwa na unywaji wa pombe. Baadhi ya magonjwa hayo ni mfarakano katika familia, maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi, unene kupita kiasi, utapiamlo hasi, mimba kuharibika, kisukari na kadhalika.

Kuna madhara ya aina mbili yanayosababishwa na ulevi. Kwanza ni kuathirika kwa mishipa ya fahamu mwilini kote kwa kupunguzwa uwezo na pili ni kuungua baadhi ya ogani za mwili hasa figo kama mlevi alikuwa mtumiaji mkubwa wa pombe kali kwani hudhoofisha kiu ngo hicho na kukifanya kushindwa kufanya kazi sawasawa au kufa kabisa au kuugua tumbo hasa vidonda vya tumbo pindi mtu anapotumia ulevi mkali.

USHAURI:

Bila shaka umefaidika na makala hizi mbili kuhusu madhara ya pombe. Kama ni mtumiaji wa pombe ni vema ukaachana nayo kwa sababu haina faida yoyote mwilini badala yake inaharibu viungo kama tulivyosoma hapa.

Leave A Reply