×

Maelfu ya Wananchi Ikungi Mashariki Wakusanyika Kumpokea Kenani Kihongosi

Maelfu ya wananchi wa Ikungi Mashariki, hususan katika eneo la Puma, wamejitokeza kwa wingi leo kumpokea Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, kabla ya kuzungumza nao katika mkutano mkubwa wa hadhara uliomaliza rasmi ziara yake ya siku tano mkoani Singida.

Wananchi hao walikusanyika mapema wakionesha hamasa kubwa, wakitumia fursa hiyo kusikiliza, kueleza kero zao pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku, zikiwemo masuala ya miundombinu, huduma za kijamii, kilimo na maendeleo ya eneo lao kwa ujumla.

Akizungumza na wananchi hao, Kihongosi aliwasikiliza kwa makini na kuahidi kuyafikisha maoni, malalamiko na mapendekezo yao kwenye mamlaka husika ndani ya Serikali na Chama, akisisitiza kuwa CCM inaendelea kuthamini sauti ya wananchi kama msingi wa maendeleo ya kweli.

“CCM ni chama cha wananchi, na ndiyo maana tupo hapa kusikiliza kero zenu, kujifunza kutoka kwenu na kuhakikisha changamoto zenu zinapata ufumbuzi wa kudumu,” alisema Kihongosi huku akiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na viongozi wao wa ngazi zote katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kulinda amani, mshikamano na umoja, akibainisha kuwa misingi hiyo ndiyo nguzo muhimu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa.

Ziara ya Kihongosi mkoani Singida imehusisha mikutano mbalimbali ya ndani na ya hadhara, mafunzo ya itikadi kwa wanachama wa CCM pamoja na kukutana na makundi tofauti ya kijamii, ikiwa na lengo la kuimarisha chama na kusikiliza kwa karibu mahitaji ya wananchi.

Mkutano wa Puma umehitimisha rasmi ziara hiyo ya siku tano, huku wananchi wakionesha matumaini mapya na imani kwa chama na Serikali katika kushughulikia changamoto zao.

Leave a Comment