The House of Favourite Newspapers

Makambo Anachinja Tu!

 

Straika Mkongomani, Heritier Makambo.

 

BAO la Straika Mkongomani, Heritier Makambo jana usiku liliipeleka Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kushinda bao 1-0 na kufikisha pointi tisa huku mashabiki nje ya Uwanja wa Taifa wakiimba wanaitaka Simba.

 

Katika mchezo huo uliochezeshwa kiumakini na Aboubakary Mtulo aliyeonekana kuumudu vilivyo, Kocha Mwinyi Zahera alikaza roho na kumtumia kipa Mkongomani, Klaus Kindoki ambaye alifanya mashabiki wengi kutulia muda mwingi na kushangilia kwa kutojiamini.

 

Kindoki kwenye mechi dhidi ya Stand alimpa hat-trick ya bure Mrundi Alex Kitenge, lakini katika mchezo wa jana alionyesha uwezo mkubwa kwa kushirikiana na mabeki wake huku Kelvin Yondani akifanya kazi kwa umakini mkubwa ili kumjengea kujiamini.

Mchambuzi maarufu Mwalimu Kashasha akizungumzia uwezo wa Kindoki alisema; “Hana uwezo wa kubadilisha presha ya mchezo kwa kubadilisha uelekeo wa mpira, jambo ambalo linakaribisha mashambulizi. Mipira ya juu usawa wa uso wake inampita kirahisi mno. Lakini naona kocha ameamua kumuamini labda tumpe muda.”

 

Bao la Makambo la dakika ya 11 akimalizia pasi ya Ibrahim Ajibu ambaye Kocha Zahera amekiri kwamba mchezaji huyo yuko kwenye fomu ambayo alikuwa akiitamani kuiona kipindi kirefu.

Mabeki wa Coastal walidhani kwamba Makambo ameotea lakini Mtulo akaita ngoma kati. Dakika ya 35, Makambo akataka kuwaonyesha ufundi wake lakini bao lake likakataliwa kwa madai kwamba Papy Tshishimbi aliyekuwa amempa pasi hiyo aliotea.

 

Yanga walionekana kujiamini zaidi katika mchezo huo na kutawala sehemu kubwa ya mchezo, lakini Makambo alilazimika kutolewa kipindi cha pili na nafasi yake kuchukuliwa na Amissi Tambwe baada ya kuumia.

Coastal Union ambao walikuwa wakijaribu kuipenya ngoma ya Yanga kwa kuwatumia kina Lyanga, Kanduru, Adeyun na Mwamnyeto lakini walionekana kukosa maarifa na uzoefu wa kuendana na kasi ya Uwanja wa Taifa hususani majira ya usiku.

 

Katika mchezo wa jana, Coastal walikuwa wanapoteza muda zaidi huku staa wao mwanamuziki Ali Kiba ambaye mashabiki walikuwa wakitarajia angecheza akiwa jukwaani.

 

Adeyum wa Coastal alimbabatiza mara kadhaa Kindoki katika kipindi cha pili na kufanya mashabiki wa Simba kuimba wanamtaka kipa huyo, Septemba 30 kwenye pambano la watani wa jadi.

 

Kikosi Yanga: Kindoki, Paulo Godfrey, Gadiel Michael, Yondani, Dante, Feitoto, Ngassa/Mateo, Tshishimbi, Makambo/ Tambwe, Ajib na Kaseke/Ninja.

Comments are closed.