The House of Favourite Newspapers

Makonda Awapa Miezi 4 Waajiri Kuwaajiri Walemavu

MKUU  wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,  leo ametoa miezi minne kwa waajiri wa makampuni na mashirika kuhakikisha wanawaajiri watu wenye ulemavu kama Sheria ya Walemavu ya 2010 na Mikataba ya Kimataifa ya mwaka 2006 iliyoridhiwa na Tanzania mwaka 2009 sura ya 27.

Amesema ifikapo Mwezi Januari mwakani ataanza ziara ya kutembelea kila kampuni na taasisi jijini Dar es Salaam kukagua kama wametekeleza sheria na agizo hilo ambapo watakaobainika kukaidi watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Amesisitiza kwamba kitendo cha kuwaajiri walemavu kitapunguza ongezeko la ombaomba, ukatili, utupwaji wa watoto wenye ulemavu, na kutahamasisha walemavu kusoma na kuwawezesha kuhudumia familia zao.

“Hatuwezi kuwa na ndugu zetu wamesoma na wanasifa za kupata kazi lakini tunawanyima, matokeo yake wengine wanaishia kujinyonga, kinamama wanatupa watoto wenye ulemavu.  Mila potovu zinaendelea kupoteza haki na mwisho wanabaki wakiwa maskini na kushindwa hata kumudu gharama za matibabu.  Jambo hili si la kufumbia macho,” alisema Makonda

Kwa mujibu wa sheria ya ajira kwa watu wenye ulemavu No. 9 ya mwaka 2010 kifungu cha 31 kinamtaka kila mwajiri mwenye wafanyakazi zaidi ya 20 kuhakikisha 3% ya wafanyakazi hao ni watu wenye ulemavu.

Comments are closed.