MSTAHIKI Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Meya wa Jiji la Shanghai la China, Zhu Huan, ofisini kwake Karimjeee Dar.
Katika mazungumzo yao, Mwita na mgeni wake wamejadili mambo mbalimbali ikiwemo namna ya kukuza na kutangaza utalii wa ndani na nje ya Dar es Salaam.
Mwita amesema jiji la Dar es Salaam lina kila aina ya vivutio vya utalii wa ndani na nje ambavyo vinaweza kuwavutia wageni mbalimbali kutoka nje ya nchi kufika jijini hapa na kutalii badala ya kwenda maeneo mengine.
Ameongeza kuwa anaamini kuwa mazungumzo hayo na mgeni wake yataleta tija na kwamba jiji la Dar es Salaam litapata watalii kutoka sehemu mbalimbali na hivyo kuliwezesha kupata mapato makubwa kupitia vivutio vilivyopo.
“Yapo maeneo mengi ambayo Watanzania hawayajui, lakini kupitia mpango huu ambao nimekuja nao hivi sasa nina imani kwamba watu ambao walikuwa wanafika kwenye jiji letu na kupanda ndege kwenda maeneo mengine, sasa watafanya utalii hapa kwetu,” amesisitiza.
Kiongozi huyo wa jiji ametumia nafasi hiyo kuueleza umma kwamba siku zijazo jiji lake linaratajiwa kupokea magari ya utalii ambayo yamenunuliwa kupitia fedha za jiji, ambapo baada ya kufika yatazinduliwa na hivyo kuanza kutumika katika kutangaza utalii wa ndani.
Kwa upande wake, Zhu Huan, amempongeza Meya Mwita kutokana na uendeshaji wake wa jiji ambapo amesema jiji la Dar es Salaam limepata meya bora.
Aliongeza kwamba anaamini kwamba ataleta mabadiliko makubwa na akaahidi kushirikiana naye katika sekta mbalimbali ikiwemo kutangaza utalii wa jiji la Dar es Salaam ili uweze kutambulika katika maeneo mengine nchini China.
Share
NA DENIS MTIMA/GPL