Mbunge Wa Wanawake Dar Aja Na ‘Tisha Mama Award’ Ukombozi Wa Mwanamke
Dar es Salaam, 30 Julai 2023: Mbunge wa Viti Maalum Wanawake jijini Dar es Salaam, Janeth Mahawanga amezindua taasisi ya Tisha Mama ambayo lengo lake kuu ni kuwakomboa wanawake wa jiji la Dar kiuchumi na kifikra ambapo kauli mbiu yake ni “Kuishi DSM ni fursa yako ya kwanza usijichukulie poa”.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mbunge Mahawanga aliwaambia kinamama hao kuwa jambo la kwanza la kujivunia kwao ni kuwa wakazi wa jiji la Dar ambapo hiyo ni fursa tosha ya kutoboa kimaisha.Taasisi ilizinduliwa kwenye hafla iliyofanyika Ukumbi wa Mlimani City jijini na kuhudhuriwa na kinamama kutoka pande mbalimbali za jiji ambapo tukio hilo lilikwenda sambamba na utoaji wa tuzo za Tisha Mama 2023.
Katika hafla hiyo wanawake kadhaa waliofanya mambo makubwa katika jamii walikabidhiwa tuzo na taasisi hiyo na wengine kushauriwa kufanya mambo kama hayo kwa maendeleo ya taifa letu. Miongoni mwa waliokabidhiwa tuzo hizo ni Mwanamama Pili Misana mwenye vituo vya kuwabadili tabia watumiaji wa dawa za kulevya ambaye amefanikiwa kuwabadili mamia ya vijana wake kwa waume na kurejea kwenye mwenendo mwema kupitia vituo vyake vya soba vilivyopo Kigamboni.
Tukio hilo lilihudhuriwa umati mkubwa wa kinamama na pamoja na viongozi wa Chama cha Mapinduzi akiwepo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Abbas Mtemvu aliyekuwa mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Mkoa wa Dar es Salaam, Khadija Said.
Wengine ni pamoja na Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Dar, Mwajabu Rajabu Mbwambo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Mzee Msengi, Wabunge, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala na wengine wengi. Kufuatia tukio hilo, mgeni rasmi alimpongeza Mbunge Mahawanga kwa kuanzisha wazo hilo la kuwanoa kinamama kifikra na kuwapa mbinu za kujikwamua kiuchumi na kuwaondoa kwenye unyonge.
Mtemvu aliendelea kumpongeza Mbunge Mahawanga kwa kutambua mchango wa kinamama waliofanya mambo makubwa katika jamii na kuwatunukia tuzo hizo za Tisha Mama. Mtemvu alimalizia kwa kuwashauri viongozi wengine kuiga mfano huo kwa ajili ya maendeleo ya jamii yetu kwa ujumla na kuwapa moyo wanaofanya vizuri wazidi kuendelea kufanya hivyo. HABARI/PICHA ZOTE NA RICHARD BUKOS /GLOBAL PUBLISHERS