The House of Favourite Newspapers

Mchele Wa Plastiki: Kama Siyo Huu Ni Nini?

0
Mkazi wa Dar es Salaam ambaye jina lake halikupatikana akionyesha kile alichodai kuwa wali wa plastiki.

HABARI kuhusu kuwepo kwa mchele wa plastiki zimekuwa zikienea miongoni mwa wananchi kila kukicha na hivyo kuendelea kuwatia wasiwasi kuhusu suala hilo, japokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) nchini imekuwa ikikanusha kwamba hakuna kitu hicho.

Uvumi au madai ya kuwepo kwa mchele wa aina hiyo unazidi kupamba moto hususan ambapo katika moja ya magazeti nchini na kwenye mitandao yamemwonyesha mwananchi mmoja aliyekuwa  akila kilichoonekana kuwa wali lakini akadai kwamba mchele uliotumika ni wa plastiki au haukuwa wa kawaida.

…Akiufinyanga wali huo ambao ulishikamana bila kusambaa au kunyumbulika mkononi mwake ambao baadaye mitandao ilimwonyesha akiubamiza chini na ukadunda kama kitenisi.

Katika video zilizoenea katika mitandao mtu huyo anaonekana akiutema mchele huo baada ya kuula.  Isitoshe, baada ya kuufinyanga  na ukagandana kama kitenisi aliubamiza chini na ukadunda kama kitenisi au mpira.

Jambo hilo ambalo limeonekana na kusikika kwa watu wengi linazidi kuwatia hofu wananchi kwamba huenda kweli kuna kile kinachoitwa mchele wa plastiki au mchele ambao si wa kawaida, yaani mchele ambao unaweza kufinyangwa na kugandana bila kusambaa, mchele ambao ukibamizwa chini hubakia umeshikana na kudunda kama mpira!

Pamoja na TFDA kila mara kukanusha kuwepo kwa kile kinachoitwa mchele wa plastiki, bado wananchi wanabakia katika giza la kutoelewa ni nini hasa kinatokea, hususan katika mazingira ya sasa ya biashara huria.

Katika mazingira haya ambayo yanawachanganya watumiaji wa chakula hicho, ni vyema juhudi  na utafiti wa kina zaidi ukafanywa na pande zote husika ili kuondoa hofu hiyo dhidi ya chakula ambacho hutumiwa na wananchi wengi nchini kila siku nchini.  Utafiti ufanywe haraka wa kuondoa wasiwasi huu wa wali ambao haunyambuliki hata unapobamizwa chini!

Ni mategemeo ya wananchi kwamba hofu hii itaondolewa mara moja ili kuepusha wasiwasi na madhara ambayo yanaweza kutokea iwapo bado hayajabainishwa.

 (STORI: WALUSANGA NDAKI | GLOBAL PUBLISHERS)

Leave A Reply