The House of Favourite Newspapers

MCHEPUKO AUA MKE KWENYE FUMANIZI DAR

Hajira Ramadhani

MWANAMKE Hajira Ramadhani (38) mkazi wa Mbagala, wilayani Temeke Dar, ameaga dunia; kilichomtoa uhai ni tukio la fumanizi.  Ijumaa limedokezwa na vyanzo mbalimbali kwamba November 3, mwaka huu saa sita mchana, Hajira alitoka nyumbani kwake kwa lengo la kwenda kumfumania mumewe aliyehisi yuko na mchepuko jirani na anapoishi.

Mmbeya anatajwa kumpenyezea ubuyu Hajira: “Mumeo yuko kwa mzee Wilfred Nyelwa na mwanamke mwingine.” Uzoefu unaonesha kwamba wanawake wengi wanapopewa ujumbe wa namna hii hupagawa na ndivyo ilivyokuwa kwa Hajira, dakika chache zilimtosha kufika eneo la tukio.

PATA MAELEZO YA AWALI KWANZA

Nyumbani kwa mzee Nyelwa kulikotokea tukio, wanaishi vijana wawili ambao ni watoto wa mwenye nyumba ambapo mkubwa anatajwa kuishi kinyumba na mwanamke aliyejulikana kwa jina moja la Fatuma ambaye anatuhimiwa kumchoma kisu Hajira na kumpotezea uhai.

Madai ya kuhusika kwa Fatuma katika tukio hilo baya yanatokana na habari nyepesinyepesi kunyetisha kwamba licha ya kuishi na mwanaume, alikuwa akituhumiwa kujivinjari na mume wa Hajira aliyejulikana kwa jina moja la Bakari.

Bakari aliyetuhumiwa na marehemu mkewe kuchepuka nje ya ndoa anatajwa kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na Fatuma baada ya kuzoeana naye kutokana na yeye kufika nyumbani kwa mzee Nyelwa kumjulia hali kaka yake aliyepanga chumba kwa mzee huyo.

SIKU YA TUKIO

Inaelezwa na chanzo kwamba siku ya tukio Bakari alikwenda kwa kaka yake ambapo inasemekana hukitumia chumba cha ndugu yake huyo kufanyia usaliti.

Wakati mwingine msemo wa za mwizi huwa haukosei, siku hiyo Bakari alipoingia kwa kaka yake, ghafla mkewe alifika hapo na kumkuta shemeji yake akiwa sebuleni huku mumewe akidaiwa alikuwa chumbani, akifanya kisichojulikana.

“Hajira alikuwa na mtoto mgongoni, alipomkuta shemeji yake sebuleni alimuuliza alipo mume wake. “Alipoona hajibiwi vizuri akamwachia mtoto yeye akaenda chumbani kwa shemeji yake ambako alipishana na mumewe akitoka mbio.

“Baada ya hapo ndiyo ugomvi ukahamia kwa Fatuma, marehemu akamuuliza; ulikuwa na mume wangu unafanya nini? “Fatuma akakimbilia chumbani kwake; Hajira alipomfuata huku akimtuhumu kumfumania ndipo alipochomwa kisu mgongoni na kupoteza maisha,” chanzo chetu kilisema.

IJUMAA LAFIKA ENEO LA TUKIO

Timu ya waandishi wetu ilipofika eneo la tukio ilifanikiwa kumpata mzee Nyelwa ambapo alisema, siku ya tukio alikuwepo lakini mwanzo wa tukio hakutilia maanani.

“Nilikuwa nimekaa zangu nje nilisikia kelele lakini kama unavyojua nyumba yenye vijana nikawa najua starehe zao, baadaye ndiyo nikaambiwa kulikuwa na ugomvi Mama Rukia (Fatuma) amefumaniwa na mume wa mtu.

“Wakati wanagombana ndiyo hayo mauaji yakatokea, tulikuwa hatuna la kufanya tuliwasiliana na vyombo vya usalama wakaja kufanya uchunguzi wao, tunasubiri watakachosema tena,” alisema mzee Nyelwa.

Kwa upande wa kiongozi wa serikali ya mtaa Kata ya Charambe ambaye ni mjumbe, Emmanuel Ambrose alisema taarifa za kutokea kwa tukio hilo wanazo, wanaendelea kushirikiana na polisi ili kukamilisha upelelezi.

MTUHUMIWA AKAMATWA

Inaelezwa kwamba mara baada ya mauaji hayo kufanyika Bakari, kaka yake na Fatuma alitoweka lakini polisi walifanikiwa kumnasa mtuhumiwa usiku aliporejea kwa lengo la kutaka kulala.

Comments are closed.