Live Kutoka Sauzi…Mishahara Mipya Simba Kufuru

SIMBA ndiyo klabu pekee kwenye Ligi Kuu Bara na Afrika Mashariki na Kati ambayo msimu ujao itakuwa na wachezaji watatu raia wa Brazil. Chukua na hili.

 

Ndiyo klabu pekee ambayo imeweka kambi Afrika Kusini kwenye hoteli ya kitajiri iliyowahi kutumiwa na timu ya Taifa ya England.

Simba imefanya mabadiliko makubwa kwenye mishahara ya wachezaji wake msimu huu ambapo mshahara mkubwa zaidi klabuni hapo utakuwa ni Sh.Mil 24 kwa mwezi. Hizo ni sawa na Dola 10,000 za Kimarekani.

 

Mmoja wa viongozi walioko ndani ya kambi ya Simba ameliambia gazeti moja makini la jijini Johannesburg kwamba, mishahara mikubwa zaidi ya wachezaji kikosini humo ni Dola 10,000.

 

Licha ya kwamba hakuweka wazi ni wachezaji gani wanalipwa mishahara hiyo lakini alisema kwamba wamejitahidi kuwapa mastaa wao maslahi mazuri kwavile wanataka kufanya mambo makubwa kwenye michuano ya kimataifa kuanzia Agosti 9.

Uchunguzi wa Spoti Xtra linaloongoza kwa mauzo kila Alhamisi na Jumapili, umebaini kwamba mastaa wanaolipwa kitita hicho ndani ya Simba ni raia watatu wa Brazil na straika namba moja Meddie
Kagere.

 

Kagere raia wa Rwanda aliongezewa dau hilo kutokana na mchango wake ndani ya Simba msimu uliopita pamoja na ofa alizokuwa nazo kutoka kwa Zamalek na Al Ahly za Misri. Simba wanafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng Sports Complex mjini Rutenburg na watakuwepo hapo kwa wiki kadhaa zijazo.

 

Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu alisema; “Tumeamua kuja kuweka kambi hapa kwavile kuna viwanja vizuri na tunaweza kupata mechi nzuri za majaribio.

“Lengo letu ni kufika mbali zaidi ya pale tulipoishia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita,” aliongeza. Simba mpaka jana ilikuwa ikipambana kupata saini ya straika Mzambia anayekipiga Orlando Pirates, Justin Shonga. Leo Jumapili ndiyo siku ya mwisho ya kukamilisha usajili wa Caf kwa kuchelewa.

 

MECHI ZA MAANA Kesho kutwa Jumanne, Simba itajipima nguvu na timu ya chuo ya Orbit College FC iliyopo nchini humo. Mechi zingine ambazo Simba itacheza kwenye kipindi hiki cha pre season, itakuwa ni dhidi ya Platnum Stars Julai ambayo itachezwa 24.

 

Kisha watavaana na Township Rollers ya Botswana (Julai 27) na ya mwisho itakuwa dhidi ya Orlando Pirates inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini itakayopigwa Julai 30.

 

MBELGIJI NA MASTRAIKA Katika kuhakikisha wanaendelea kuwa imara katika msimu mpya ujao, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems amewafungia kazi washambuliaji wake kwa kufanya zoezi maalum la ufungaji mabao katika mazoezi ya juzi. Simba juzi ilifanya mazoezi yake maalum ya ufungaji wa mabao kwa wachezaji wake ili kuhakikisha msimu ujao wanafunga mabao mengi zaidi kwenye mechi zao .

 

Msimu uliopita Simba ilifunga jumla ya mabao 77 huku Meddie Kagere akiibuka kinara kwa kufunga mabao 23 kwa msimu uliopita.

 

Aussems msimu ujao atakuwa na washambuliaji makini kama Kagere, Ibrahim Ajibu, Wilker Henrique, Francis Kahata, John Bocco na Clatous Chama ambaye alikuwa mpishi mzuri wa mabao katika msimu uliopita.

 

Katika mazoezi hayo kocha huyo alifanyia kazi eneo hilo la ufungaji mabao kwa kuwa walitumia takribani wachezaji wake wote ili kuangalia uwezo wao. Ambapo mabeki, viungo na washambuliaji walifanya zoezi hilo ili kuona anawapika vipi wachezaji wake kuelekea msimu mpya.

 

Kwenye zoezi hilo wachezaji baadhi ambao walionekana kufunga mabao ni pamoja na kiungo mpya Francis Kahata, Clatous Chama, beki Gerson Fraga, Sharaf Eldin Shiboub huku Tshabalala akibutua nje.


Loading...

Toa comment