The House of Favourite Newspapers

Mkwasa Afanya Kikao Kizito na Mafaza Yanga SC

BAADA ya kuanza majukumu yake kwenye kikosi cha Yanga, Kaimu Kocha Mkuu, Charles Boniface Mkwasa juzi alitumia saa mbili kufanya kikao na wachezaji wake wote na kikubwa aliwataka kutambua ukubwa na thamani ya kuichezea klabu kubwa, Yanga.

 

Kocha huyo alirithi kibarua hicho juzi mara baada ya uongozi wa Yanga kumsitishia mkataba aliyekuwa kocha wake Mkongomani, Mwinyi Zahera kabla ya Mkwasa kukaimu nafasi hiyo.

 

Mkwasa jana alianza kukaa kwenye benchi la timu hiyo rasmi wakati walipocheza na Ndanda FC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Stori na Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, kikubwa kwenye kikao hicho kocha huyo aliwahakikishia wachezaji kuwa mengi mazuri yatakuja Yanga kama watacheza kwa kujituma na kujitolea kwa moyo mmoja uwanjani na kupata matokeo mazuri ya ushindi.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kikao hicho walikaa juzi mara baada ya chakula cha usiku walipotua Mtwara na Mkwasa aliwataka wachezaji hao kufahamu wapo Yanga kwa ajili ya kuchukua makombe na siyo kingine, hivyo ni lazima washinde kila mchezo wa ligi wa mbele yao kwa kuanzia na Ndanda.

“Mkwasa amewaambia wachezaji hao hawana sababu ya timu kutopata matokeo mazuri, kwani kila mchezaji aliyesajiliwa ni bora na ana vigezo vya kuichezea Yanga ambayo ni klabu kubwa Afrika, hilo lipo wazi hivyo ni lazima kila mmoja aipambanie timu yake ambayo ndiyo inayomlipa mshahara.

 

“Wote walisajiliwa na Yanga kwa sababu walionyesha ubora wakiwa kwenye timu zao huko walipotoka baada ya kuonekana wana sifa ya kuichezea timu hii. Jukumu lake ni kuwasaidia ili watimize malengo ya timu.

“Wametakiwa kufahamu wapo hapa kuipigania klabu hii na kubeba vikombe, hilo ndio lengo kuu kwa kila mchezaji anayeitumikia klabu hii, hivyo wanapaswa kuishi katika utamaduni huu na ili kutimiza dhamira hii ni lazima waanze kushinda michezo yetu.

 

“Anaamini watakaposhinda kila kitu kitarejea katika hali yake, uwanja utajaa na furaha kwa mashabiki itarejea Yanga na wao watapata fedha kwa ajili ya familia zao wenyewe kwa wale wakongwe waliokuwepo muda mrefu wanafahamu hilo,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Aidha alipotafutwa Mkwasa kuzungumzia hilo alisema: “Ni kweli nilifanya kikao na wachezaji kama ulivyo utamaduni wa makocha wote mara baada ya kukabidhiwa timu mpya.

“Nilijaribu kuwarejesha katika hali ya kawaida kwa maana ya kuwajenga kisaikolojia baada ya kocha wao kuondolewa, hivyo tumezungumza mengi na kikubwa kukumbushana majukumu ya timu, hivyo nimejisikia furaha wachezaji wote nimewaona wapo vizuri na wepesi kuelewa.”

Comments are closed.