The House of Favourite Newspapers

MPANGAJI AMSULUBU MTOTO WA MWENYE NYUMBA!

0
MPANGAJI AMSULUBU MTOTO
Mtoto wa mwenye nyumba, Aidath Ramadhani .

Mwanadada ambaye ni mpangaji aliyetajwa kwa jina la Magdalena Chata, anadaiwa kumsulubu mtoto wa mwenye nyumba, Aidath Ramadhani ambaye aliachiwa mamlaka ya usimamizi wa nyumba wanayoishi maeneo ya Kinondoni jijini Dar.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo la hivi karibuni, Magdalena anadaiwa kumpiga mtoto huyo na jalo la kuopolea maandazi, kisa kikiwa ni moto aliokuwa akiuwasha mpangaji huyo. Akilisimulia Ijumaa Wikienda mkasa mzima, Aidath alisema kuwa, anakumbuka siku ya tukio hilo Julai 30, mwaka huu ambapo mpangaji wake huyo alikuwa ndani akifanya shughuli zake, naye akatoka nje ya chumba chake kisha akawasha moto.

 

Alisema kuwa, baadaye aliingia ndani, lakini alipotoka, alipigwa na butwaa kukuta moto aliouwasha umezimwa na maji na aliyeuzima ni Magdalena. Alisema kuwa, kitendo hicho hakukifurahia hivyo alimpigia simu mume wa mpangaji huyo na kumueleza tatizo lililopo nyumbani hapo.

“Nilipompigia simu mumewe akaniambia hawezi kunisaidia chochote kwa sababu alikuwa mbali. Ndipo nikaona isiwe tabu, nikaamua kuwasha tena moto kwani sikutaka matatizo na mtu,” alisema Aidath.

Majeruhi huyo alisema kuwa, alipokuwa akijaribu kuwasha moto, Magdalena alitoka ndani na kumweleza kuwa siku hiyo moto hautawaka kwani yeye aliamua hivyo na kuanza kumnyang’anya jiko akitaka kuumwagia maji moto.

 

MPANGAJI AMSULUBU MTOTO
Aidath Ramadhani .

 

“Tulinyang’anyana sana jiko bila mafanikio, ndipo mwenzangu akaamua kunipiga na jalo kwenye paji la uso na kunisababishia jeraha kubwa,” alisema Aidath akionesha jeraha bichi usoni. Aidath alisema kuwa, baada ya kitendo hicho alikwenda kuripoti kwenye Kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar na kumfungulia kesi yenye jalada namba OB/RB/11307/2017 – KUJERUHI ambapo mtuhumiwa alikamatwa na kulala selo kwa siku moja kabla ya kuachiwa kwa dhamana.

“Tuliambiwa tutapangiwa siku ya kwenda mahakamani kwa ajili ya kesi yetu kuanza kusikilizwa,” alesema Aidath. Ijumaa Wikienda ilimsaka Magdalena nyumbani hapo lakini hakupatikana.

Ilidaiwa kuwa, huwa anakwenda kazini kwake, Tegeta, lakini hata simu yake haikupatikana hadi tunakwenda mtamboni hivyo gazeti hili linaahidi iwapo Magdalena atapatikana, naye ataanika ya kwake ili kuleta uwiano wa habari hiyo.

Kwa mujibu wa Aidath, ugomvi wote huo uliotokea ulijengwa na chuki ya siku nyingi kwani wawili hao hawakuwa na uhusiano mzuri. “Mwenyewe alisema kuwa, eti nikiwasha moto, moshi unaenda kwenye nguo zake, lakini kiukweli mimi na huyo mpangaji hatukuwa na uhusiano mzuri. “Hata hivyo, baba yangu ambaye ndiye mwenye nyumba, amekuja kwa ajili ya kesi hiyo, kwa hiyo huenda mpangaji huyu akahamishwa kwa kupewa notisi,” alisema Aidath.

STORI: HAMIDA HASSANI NA GLADNESS MALLYA| IJUMAA WIKIENDA

 

Usipitwe na Matukio, Install ===>Global Publishers App

Sikiliza Hadithi za Mtunzi Eric Shigongo Hapa

Leave A Reply