MREMBO: SANCHEZ ALINITONGOZA NIKAMKATAA

Alexis Sanchez

NATALIA Mandiola, ni mtangazaji wa runinga katika idara ya michezo, amefunguka kuwa nyota wa Manchester United, Alexis Sanchez alitupa ndoano kwake lakini akaipangua. Amefunguka kuwa staa huyo alimtupia ndoano kwa gia ya kumualika nyumbani kwake.

 

Natalia ambaye ni mtangazaji wa michezo nchini Chile, ambapo ndipo anapotokea Sanchez, ameyasema hayo ikiwa ni siku chache tangu mchezaji huyo aonekane akiwa na msichana mwingine mtaani.

Sanchez ambaye analipwa mshahara wa pauni 505,000 (Sh bilioni 1.3) kwa wiki, alimpigia simu Mandiola baada ya kupata namba yake kutoka kwa rafiki wa mrembo huyo, ikiwa ni siku moja baada ya wawili hao kukutana kwenye ukumbi wa muziki.

 

Mandiola, anayetangaza katika Kituo cha TVN, anasema Sanchez mwenye umri wa miaka 30, alimpigia simu na kuanza kushuka ‘mistari’ kikubwa ikiwa ni kumuomba afike nyumbani kwake kesho yake.

 

Baadaye alikazia ujumbe wake huo kwa kumtumia ujumbe mfupi wa maandishi akimsisitiza juu ya kufika nyumbani kwake. Mandiola anasema: “Kuna kitu sikukipenda, alinikaribisha nyumbani kwake, kwangu mimi yeye alikuwa mgeni, nilikataa kwa kuwa siwezi kwenda kirahisi nyumbani kwa mtu mgeni.”

Ameongeza kuwa, tukio hilo lilitokea siku za nyuma wakati Sanchez akiwa singo baada ya kuachana na aliyekuwa mpenzi wake, Mayte Rodriguez, mwaka jana. Inaaminika kwa sasa Sanchez ana mpenzi mpya japokuwa hajawa tayari kumuweka wazi. Wawili hao walionekana pamoja katika kituo cha treni cha Wimslow jijini London.

MAJANGA JUU YA MAJANGA

Upande wa pili ni kuwa, Sanchez amekuwa na maisha magumu uwanjani tangu atue ndani ya Man United akitokea Arsenal mwaka mmoja na nusu uliopita, akiwa anajiandaa na msimu mpya 2019/20 amekutana na sakata lingine. Mkongwe huyo alitibuana na chipukizi, Mason Greenwood wakati wakiwa mazoezini na kujikuta wakirushiana maneno.

 

Ilikuwa hivi, Sanchez alichelewa kufika katika kambi ya mazoezi kutokana na kupewa muda wa kupumzika zaidi, alipofika akaanza mdogomdogo na mwisho akapata nafasi ya kucheza na wachezaji vijana ambapo huko ndipo wakatibuana na Greenwood mwenye umri wa miaka 17.

 

Kinda huyo alimchezea faulo Sanchez ambaye alikasirika na kujikuta akianza kumuwakia mwenzake kwa kuwa ndiyo kwanza anarejea kutoka kwenye majeraha na alikuwa akijiweka fiti mdogomdogo kwa ajili ya msimu mpya.

 

NJIANI KUUZWA

Wakati akiwa bado hajakaa sawa, inadaiwa kuwa kocha wa timu yake, Ole Gunnar Solskjaer yupo tayari kumruhusu Sanchez aondoke klabuni kwa kuwa hana nafasi katika kikosi cha kwanza.

 

Klabu ya AS Roma ndiyo pekee ambayo inamtaka na kwa sasa anafanya mazoezi na kikosi cha wachezaji wa akiba wa Man United ili ajiweke fiti. Kikwazo kikubwa ni mshahara wa mchezaji huyo ambao ni mkubwa na Roma hawako tayari kumlipa kwa kiwango kilekile anacholipwa Man United


Loading...

Toa comment