The House of Favourite Newspapers

Msekwa: Wakati wa Kupinga Matokeo ya Urais Mahakamani Umeshafika

0
Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Pius Msekwa.

Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Pius Msekwa amesema wakati wa kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais mahakamani umeshafika na kilichobaki ni kupitisha rasimu ya Katiba ambayo ina ibara inayotoa haki hiyo.

 

Msekwa, ambaye pia alikuwa makamu mwenyekitiwa CCM, ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili kuhusu hatua ya Mahakama Kuu ya Kenya kubatilisha uchaguzi wa rais wa nchi hiyo uliofanyika Agosti 8 baada ya mgombea wa upinzani kufungua kesi, akidai kulikuwa na ukiukwaji wa sheria.

 

Kwa uamuzi huo, ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta, anayewania kuongoza taifa hilo kwa kipindi cha pili mfululizo, umebatilishwa na sasa atapambana tena na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga wa muungano wa NASA.

 

Wakati ibara ya 140 ya katiba ya Kenya inaruhusu mtu yeyote kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais mahakamani ndani ya siku saba tangu kutangazwa kwa mshindi, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakataza.
Ibara ya 74(12) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema hakuna mahakama yoyote nchini itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi (NEC) katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba.

 

Hilo ni jambo ambalo limekuwa likijadiliwa tangu kubatilishwa kwa uchaguzi wa rais wa Kenya, lakini alipoulizwa kuhusu suala hilo, Msekwa muda umefika.
“Jibu ni ndiyo,” alisema Msekwa.

“Tunaweza kufikia hatua hiyo na tumeshaifikia. Katiba Mpya iliyopitishwa na Bunge mwaka 2014 inasema matokeo ya urais yanaweza kupingwa mahakamani.
“Katiba ya sasa hairuhusu, lakini katiba inayopendekezwa imeruhusu. Tunachosubiri ni referendum (kura ya maoni) tu.”

Mchakato wa kubadili Katiba ulianzishwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwaka 2011 lakini ukakwama mwaka 2014 ukiwa katika hatua ya kura ya maoni baada ya NEC kueleza kuwa haikuwa na muda wa kutosha .

Hata hivyo, mchakato huo uliingiwa na dosari baada ya baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba, hasa kutoka vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD kuususia wakidai kuwa chombo hicho kiliacha Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuingiza ajenda za chama tawala.
Hata hivyo, wajumbe waliosalia waliendelea na mchakato na kupitisha Katiba Inayopendekezwa.
Hata hivyo, Rais John Magufuli ameshasema kuwa Katiba mpya si kipaumbele chake kwa kuwa kwa sasa anataka “kuinyoosha nchi”.

Kuhusu suala hilo, Msekwa alisema hawezi kuzungumzia utawala wa sasa kwa kuwa una utendaji wake.
“Mambo ya utawala wa sasa siwezi kuyasemea,” alisema Msekwa.
“Swali lako la msingi ni kama tunaweza kufikia hatua ya kupinga matokeo ya urais na nimesema ndiyo tunaweza.”
Kada mkongwe wa CCM aliyewahi kuwa waziri katika utawala wa Mwalimu Julius Nyerere na ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini, alisema hata kabla ya kupata Katiba mpya vyama vya upinzani vilishakubaliana na Kikwete mambo manne, likiwemo la kupinga matokeo ya urais.

“Wagombea urais kupingwa mahakamani ni jambo zuri, “ alisema.
“Kimsingi vyama vya upinzani na na Rais Kikwete walishakubaliana baada ya mchakato wa Katiba kukwama. Sijui kwa nini hayakutekelezwa.
“Mambo manne waliyokubaliana ni kupinga matokeo ya urais, mgombea urais atangazwe kushinda akifikisha asilimia 50 na zaidi ya kura, kuwa na tume huru ya uchaguzi na kuwa na mgombea binafsi. walikubaliana kabisa, sijui kwa nini hayakutekelezwa. Waulize wapinzani.”

 

Kwa upande wake Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Mohamed Bakari alisema ili Tanzania ifikie mabadiliko ya Kenya, ni lazima mapambano ya kudai Katiba mpya yaongezeke.
“Ukichukua uzoefu wa Kenya, mpaka katiba imepatikana kulikuwa na mapambano makali sana yakihusisha vyama vya siasa, asasi za kiraia na wananchi wanaopenda demokrasia. Msukumo kama huo ni mdogo Tanzania,” alisema Dk Bakari.
Kwa upande wake, Njelu Kasaka, waziri wa zamani enzi za utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, alisema ili kufikia mabadiliko ya Katiba ni lazima wananchi wenyewe waidai.
“Nawapongeza Wakenya kwa sababu wameweza kujitawala kwa kuweka uongozi wanaoutaka na kuuondoa wenyewe. Sisi tunaweza kufikia hatua hiyo kwa kudai Katiba nzuri na kuweka taasisi zitakazoisimamia, kama Bunge na Mahakama,” alisema Kasaka.

 

Alisema licha ya Tanzania kuwa mstari wa mbele katika vita ya ukombozi wa Afrika miaka ya sitini, imebaki nyuma kidemokrasia tofauti na nchi zilizokuwa nyuma.
“Tuliwalaumu makaburu wa Afrika Kusini kwa kukandamiza demokrasia, tukasema demokrasia itawale hadi Zimbabwe, lakini leo tumeshindwa kuwawajibisha viongozi wetu,” alisema.
“Wananchi waanze kudai Katiba mpya, lakini hatuwezi kuifikia kama hatuna kambi ya upinzani imara. (Kama) Bado hatujawa na vyama vya upinzani imara, kwa sababu kwa sasa vinabanwa na bado wananchi wengi hawaonyeshi mwamko. Lazima tusawazishe nguvu ili kupata mabadiliko.”

Chanzo: Mwananchi

Global Tv Kenya: Hotuba ya Rais Uhuru Kenyatta – Tuko tayari kwa uchanguzi tena

Leave A Reply