MSHTUKO: MSANII BONGO MUVI APIGWA RISASI
MACHOZI! Msanii ambaye ni mwigizaji mwanamama wa Bongo Muvi, Leyness Ngunguye amefariki dunia akiwa kwenye dimbwi la damu baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana nchini Afrika Kusini ‘Sauz’.
Tukio hilo lililoacha simanzi nzito kwa Watanzania waishio nchini humo lilijiri hivi karibuni maeneo ya Mgahawa wa Nando’s jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
LEYNESS NI NANI?
Leyness ni Mtanzania aliyekuwa anapeperusha bendera ya Bongo Muvi nchini Afrika Kusini tangu miaka ya 2000 huku kazi zake na wenzake zikisambazwa na Kampuni ya Steps Entertainment yenye makao yake hapa nchini. Leyness alianza kazi hiyo mwaka 2000 nchini humo ambapo kazi yake ya kwanza iliyomtambulisha kwenye ulimwengu wa filamu ni Bad Friend aliyoigiza kama dada wa uswahilini.
Katika sinema hiyo, Leyness alitumia jina la uigizaji la Emmy akiwa na washiriki wengine hapa Bongo kama Ummy Wenslaus ‘Dokii’, Dadi Ramadhan, Ashura Ng’anga, Maximilian Bushoke na Fortunatus Kasomfi. Msanii huyo pia alishiriki utengenezwaji wa Sinema ya My Nephew akiwa kama mwongozaji mkuu.
NDUGU ASIMULIA
Akisimulia kwa machungu kifo hicho baada ya mazishi ya Leyness yaliyofanyika mapema wiki hii Chamazi jijini Dar, ndugu wa marehemu aliyekuwa akiishi naye Afrika Kusini, Dalini Ngunguye alieleza kisa na mkasa wa kusikitisha. Dalini alisema kuwa, anakumbuka ilikuwa mchana ambapo dada yake huyo alimuaga kwamba anaelekea sehemu iitwayo Nando’s.
Alisema alipomuuliza anakwenda kufanya nini, alimwambia anakwenda kufanya ‘shopping’ ya vitu vyake mbalimbali. Dalini alieleza kuwa, Leyness aliondoka nyumbani na mmoja wa marafiki zake wa karibu ambaye ndiye walikuwa wakipenda kutoka wote mara kwa mara.
Dalini alisema: “Ilikuwa hivyo, lakini baada ya muda nilipata taarifa ya kunidanganya kuwa dada yangu amepatwa na tatizo la presha ghafla. Hawakutaka kuniambia amepigwa risasi. “Nilitoka nikaelekea hospitalini alikofikishwa kwa ajili ya huduma ya kwanza na baadaye kutaka kumuona ndipo nilielezwa kuwa itakuwa ngumu kutokana na hali yake kuwa mbaya.
“Niliendelea kusubiria ili nifanikiwe kumuona, lakini muda mfupi nilipatiwa taarifa kwamba ameshafariki dunia kutokana na kutokwa na damu kwa muda mrefu kufuatia jeraha la risasi aliyopigwa mguuni kisha akatokwa damu nyingi zilizotengeneza dimbwi baada ya kuanguka chini.
TAARIFA YA KIFO
“Nilipopata taarifa ya kifo chake sikukubali kwa urahisi ndipo nikambana sana rafiki yake ambaye ndiye aliyekuwa naye siku nzima hadi nilipotaarifiwa kuwa amepatwa na presha ghafla.
“Nilijaribu kumuuliza kwa hisia ya tofauti ndipo aliponiweka wazi kuhusiana na ishu ilivyotokea kuwa walipokuwa mjini walivamiwa na watu wasiojulikana na katika kupambana kujiokoa ndiyo walimpiga Leyness risasi mguuni.
“Alisema baada ya kupigwa risasi alianguka, akawa anatokwa na damu nyingi sana zilizosababisha kuloa chapachapa kisha kukimbizwa hospitalini kwa msaada wa wasamaria wema ambako hakukaa sana kwani alifariki dunia.”
TOFAUTI NA RAFIKI
Dalini aliendelea kueleza kuwa, baada ya kupata taarifa hizo za kina alikumbuka nyuma kwamba dada yake alishakuwa na tofauti na mmoja wa marafiki zake ambaye alishamweleza kuwa kuna wakati anamtumia ujumbe mfupi (SMS) wa vitisho.
“Nilijaribu kumshawishi aende kwenye vyombo vya sheria na nilikuwa ninamweleza hivyo mara nyingi sana kila aliponionesha ujumbe wa kutumiwa na huyo rafiki yake.
“Lakini yeye aliishia kutoa kauli ya kusema anamwachia Mungu ndiye anayejua kwani ndiye mpangaji wa kila jambo,” alisema ndugu huyo wa marehemu.
Aliendelea kusema kuwa, baada ya yote hayo kutokea, aliwasiliana na familia yao iliyopo Tanzania pamoja na dada yake mkubwa anayeishi nchini Kenya na wasanii wa filamu aliyokuwa nao nchini humo kwa ajili ya maandalizi ya kusafirisha mwili kuja Tanzania.
“Ninashukuru kwa kweli nilipata ushirikiano mzuri wa Watanzania waishio nchini Afrika Kusini na kufanikiwa kusafirisha mwili kutoka Afrika Kusini hadi Tanzania hadi kufanikisha safari yake ya mwisho,” alisema Dalini na kuongeza:
“Leyness alianza mambo ya muvi katika Kikundi cha Kilimanjaro Feature akiwa kama mdada aliyekuwa na kipaji huku akiwa amekosa pa kukiwakilisha.”
MWIGIZAJI MWENZAKE
Naye mmoja wa Watanzania ambaye ni mwigizaji anayeishi nchini Afrika Kusini, Fortunatusi Kasomfi alisema kifo cha Leyness ni pigo kwani walikuwa wamefikia hatua ya kujiendesha wao kama wao na kuondokana na mambo ya kusimamiwa na kampuni za filamu.
“Sina mengi ya kuongea, kubwa nimuombea kwa Mungu mwenzetu aliyetangulia, yote ni kazi ya Mungu. Ni pigo kubwa sana kwani tulikuwa na malengo ya kufika mbali kwa kazi yetu hasa ukizingatia tunatumia Kiswahili tukiwa nchi ya watu wengine,” alisema Kasomfi.
Alisema tayari walishaanzisha kampuni ijulikanayo kwa jina la Forjoys Production Ing ya kusimamia kazi zao kwa kuwa kampuni ya Tanzania iliyokuwa ikisambaza kazi zao ina changamoto zake.
AMEACHA WATOTO 3
Leyness ambaye aliolewa na mwanaume raia wa Afrika Kusini ameacha mume na watoto watatu, mmoja wa Kike.
Stori: Zaina Malogo, Ijumaa
Comments are closed.