The House of Favourite Newspapers

MTANDAO HATARI WA WANAWAKE WABAINIKA!

UKISIKIA aibu, fedheha na dhihaka subiri ufumaniwe! Usiombe tukio hilo likutokee, endelea kusikia stori kwa watu.

Lakini maumivu zaidi ni pale utakapogundua kuwa kufumaniwa kwako ni mchezo mchafu wa kitapeli, Ijumaa Wikienda linakupa zaidi.

MTANDAO HATARI

Gazeti hili limebaini kuwepo kwa mtandao huo hatari wa wanawake wanaotumika kuwatega wanaume kimapenzi, kuwadhalilisha na kutapeli mamilioni ya fedha.

 

MCHEZO ULIVYO

Chanzo chetu cha habari kilichoomba hifadhi ya jina, kilifika ofisini kwetu kikiwa na folda lenye picha za fumanizi kati ya mwanaume mmoja aliyetajwa kuwa mfanyabiashara wa jijini Dar na mke wa mtu.

Ni kweli, picha zilionesha mwanaume akiwa chini ya ulinzi wa askari, mikono ikiwa na pingu huku akiwa na mwanamke kitandani, akiwa amejifunika kwa taulo na mwanamke shuka.

Baada ya maelezo ya awali kati ya sosi huyo na Ijumaa Wikienda, tulikubaliana kupewa muda wa kufuatilia ili kujiridhisha ukweli wa tukio hilo ambapo chanzo hicho kilitoa namba za simu za mke aliyefumaniwa, mume na jamaa aliyefumaniwa.

 

Mwandishi wetu akamvutia waya anayeelezwa kuwa ni mume wa mwanamke aliyefumaniwa ili kumpa nafasi ya kutoa maelezo ya msingi, lakini iliita bila kupokelewa.

Katika hatua nyingine, namba ya mwanamke aliyedaiwa kufumaniwa na mumewe, haikupatikana muda wote ilipopigwa.

Wote wawili walitafutwa kwa siku tatu mfululizo na hali iliendelea kuwa hiyohiyo; ndipo timu yetu ilipoanza kuingiwa na shaka juu ya tukio hilo.

 

MTANDAO WAFUMUKA

Makachero wa Ijumaa Wikienda waliamua kumsaka mwanaume anayedaiwa kufumaniwa ambapo walifanikiwa na bwana huyo kutoa ushirikiano.

Awali, alipopatikana na kuelezwa uwepo wa picha zake za fumanizi katika chumba chetu cha habari, jamaa huyo (tunahifadhi jina lake kwa sababu maalum) alihamaki kidogo kisha akauliza: “Gazetini? Umesema wewe ni mwandishi wa habari? Okay… sasa nimeshaelewa vizuri kinachoendelea.”

Alipoulizwa sababu za kusema hayo, hakujibu badala yake naye akauliza: “Si umesema mnazo hizo picha hapo? Naweza kuona moja ambayo mimi naonekana?” Akajibiwa ndiyo, akaomba atumiwe, zoezi ambalo lilifanyika mara moja kupitia Mtandao wa Kijamii wa WhatsApp.

 

Kabla ya dakika moja kupita, mawasiliano ya simu kwa njia ya WhatsApp, kati ya kachero wetu wa Kikosi cha Kufichua Uovu (OFM) cha Global Publishers na bwana huyo yakionesha ameshaona picha aliyotumiwa, mshukiwa huyo alipiga simu.

“Ni kweli ndugu yangu… nalitambua hili tukio, lilitokea kama wiki tatu nyuma, lakini ni tukio la kutengenezwa. Nimetapeliwa fedha zangu na hao jamaa kwa kujifanya wamenifumania,” alisema.

 

AANIKA UCHAFU WOTE

Katika maelezo yake, bwana huyo alisema amefahamiana na mwanamke huyo miezi miwili iliyopita, walipokutana kwa mara ya kwanza jijini Tanga, alipokwenda kikazi.

“Huyo dada ni mtu wangu. Ile siku nilikuwa nimelala naye kwa mara ya pili; mara ya kwanza ilikuwa Tanga. Nilikwenda kikazi, yeye akasema amekwenda kwenye semina ya kazini kwao.

 

“Tulikutana kwenye starehe, kama unavyojua tena tukayajenga, tukaondoka pamoja kwenda hotelini. Tangu hapo tukawa tunawasiliana,” alieleza.

Alisema, baada ya kudumisha uhusiano wao wa simu kwa muda mrefu, wakapanga kukutana tena siku ya tukio ndipo akakutana na balaa ambalo hawezi kulisahau maishani mwake.

 

SIKU YA TUKIO

Jamaa huyo aliendelea kufunguka: “Tulikutana katika baa moja Msasani…kama kawaida tumekula na kunywa kisha tukaingia chumbani. Ilikuwa kwenye saa tano na dakika usiku. Mwenzangu alikuwa bize sana na simu akiwasiliana na watu kwa meseji.

 

“Baadaye akaniomba simu yangu awasiliane na nyumbani, nikampa. Lakini akasema hawapokei, mara mlango ukagongwa. Wakaingia watu wanne; kati yao askari wawili, mhudumu wa ile lodge wa kike na mwanaume aliyesema amenifumania na mkewe.

“Alifikia kumpiga yule mwanamke makofi mawili ya usoni, yule mwanamke akawa analalamika; baba Sara kwa nini unanifanyia hivi? Nikawa sielewi…nikafungwa pingu, wakati huo kuna mtu alikuwa akipiga picha za tukio.”

 

APELEKWA POLISI

Akiendelea kusimulia tukio hilo, jamaa huyo ambaye amekiri kuwa na mke na watoto watano, alisema alichukuliwa hadi katika kituo kimoja cha Polisi kilichopo wilayani Kinondoni, lakini hakuingizwa ndani, akatakiwa kutoa shilingi milioni 6 ili mambo yaishe.

“Sikuwa na hiyo fedha, nikawaambia nina laki sita kwa muda ule kwenye simu, wakasema niirushe kwa yule mwenye mke. Wakaniachia kwa ahadi kwamba kesho yake nikamilishe shilingi milioni 3 anisamehe, nikakubali ili mambo yasifike Polisi,” alisema.

 

Alisema, kesho yake asubuhi alituma shilingi 400,000 na kuomba mambo yaishe, lakini mwenye mke akamwambia aongezee japo shilingi 500,000.

“Wakati huo niliwasiliana na mama Sara, akasema ameshamtumia 500,000 kwa simu kwa kupitia wakala, kwa hiyo nimwambie jamaa ni mimi nimetuma, kwa hiyo akataka laki tano nyingine ili kukamilisha shilingi milioni mbili.

 

“Cha kushangaza baadaye nikapigiwa na jamaa aliyekuwa akipiga picha, akaniuliza kama nimeshatoa fedha, nikamwambia nimetoa milioni na nusu, akasema hajapewa mgawo wake, kwa hiyo atapeleka picha gazetini,” alisema jamaa huyo mkazi wa jijini Dar.

Hapa anazungumzia msumari wa mwisho: “Huu ni utapeli, maana mama Sara aliniambia mapema kuwa ana mtoto na bwana aliyezaa naye, alishaachana naye muda mrefu, kila mmoja anaishi kivyake.”

 

NENO LA MHARIRI

Timu yetu bado ipo kazini kuchimbua mkasa huu kwa kuwapata mama Sara na mwanaume anayedaiwa kuwa mumewe ambaye alimfumania jamaa huyo.

Wanaume mnapaswa kuwa makini, kwani ukiingia katika mtego huu utadhalilika, utasononeka na zaidi utatapeliwa kiasi kikubwa cha fedha.

STORI: WAANDISHI WETU, DAR

JPM Amewataja Hadharani Matajiri Wanaoibia serikali

Comments are closed.