The House of Favourite Newspapers

MWANAFUNZI ATOWEKA SIKU 30, APATIKANA, AFARIKI

Khadija Ally Masoud enzi za uhai wake.

MWANAFUNZI wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Mikocheni B, Khadija Ally Masoud (15), amefariki dunia Jumamosi iliyopita baada ya kutoweka nyumbani kwao Mwanyamala jijini Dar mwezi mzima akitokea shuleni.

Akizungumza kwa uchungu na mwandishi wetu juzi, mama mzazi wa mtoto huyo, Shuena Salum alisema kuwa, mtoto wake huyo alienda shuleni kama anavyofanya kila siku, lakini siku 30 zilizopita hakurejea nyumbani.

 

Akiendelea kuuelezea mkasa huo Shuena alisema, baada ya kuona mtoto wake hakurudi nyumbani siku hiyo walianza kumtafuta sehemu mbalimbali mpaka shuleni na kwenye vyombo mbalimbali vya habari.

“Siku ambayo hakurudi nyumbani tulianza kumtafuta sehemu mbalimbali zikiwemo hospitali, tukatoa taarifa polisi lakini hatukupata mrejesho wowote.

 

Mjomba.

 

“Ilibidi twende Kituo cha Polisi Kijitonyama ambako tulitoa taarifa na kufunguliwa jalada namba OB/ RB/1198/018 kisha jalada la uchunguzi namba KJN/ CID/PE. 17/ 018,” alisema mama huyo.

Aliongeza kuwa wakati wakiendelea kumtafuta katikati ya wiki iliyopita walipata taarifa kutoka Kituo Kidogo cha Polisi cha Mtambani kwamba kuna mtoto katangazwa msikitini amepotea, wakatoa namba za simu za huyo mtu aliyenaye aliyeko Morogoro ambaye alitajwa kwa jina la Gordon Mtemi.

Aliendelea kusema kuwa baada ya kusikia hivyo walichukua hiyo namba na kuanza kuipiga ambapo mtu huyo alijitambulisha kwa jina la Gordon Mtemi na kudai kuwa, alikutana na mwanaye kwenye basi la kwenda Morogoro na alikuwa hajui anakoenda hivyo alimchukua mpaka nyumbani kwake.

 

 

“Yaani huyo kaka nilipompigia simu akaniambia mtoto yuko naye ila anaumwa sana na ameshatumia fedha zake shilingi 170,000 kwa kumtibu, hivyo akasema twende tukamchuku ila yeye hayupo kaenda vijijini.

“Aliniambia amemuacha mwanangu na mkewe nyumbani kwake hapo Morogoro mjini,” alisema mama huyo.

 

Aliongeza kuwa, kwa vile kuna mdogo wake Morogoro, alimwambia naye akaenda alipo mtoto na alimkuta akiwa hoi kwa ugonjwa na alikuwa analia kwa maumivu, hivyo alimchukua na kumleta Dar, ambapo walifika majira ya saa sita usiku.

 

 

 

“Mwanangu alifika akiwa hoi huku analia tu, hivyo tulimpeleka moja kwa moja Hospitali ya Mwananyamala, madaktari walipompima walimkuta ana damu mbili tu hivyo walimlaza, ambapo majira ya saa tisa mchana alifariki dunia,” alisema mama huyo huku akilia.

 

Gazeti hili liliwasiliana na Gordon ambaye alikiri kumchukua mtoto huyo hadi nyumbani kwake kwa kuwa alikutana naye kwenye basi akielekea Morogoro.

“Nilimhoji unakwenda Morogoro kwa nani akasema anakwenda tu huko kwa kuwa anaoishi nao, aliodai ni shangazi yake Husna na bibi yake Zuwena wanamtesa.

 

 

“Nilimfikisha kwa Bi Mkubwa lakini baadaye nikampeleka nyumbani kwangu lakini akawa anaumwa kila siku. Ikabidi tumpeleka hospitali wakasema ana tayfodi na malaria.

“Tulimuuliza kama ana namba ya simu ya mama yake au ndugu zake akasema hana. Nilimuuliza Dar anaishi wapi, akasema Kinondoni Ukawa ndipo nilipofunga safari kwenda hapo na nikatoa namba yangu ya simu Kituo cha Polisi Mtambani na msikitini ili itangazwe na tujuwe wazazi wake walipo,” alisema Gordon.

 

Afisa mmoja wa Kituo cha Polisi Kijitonyama ambaye aliomba jina lake kuhifadhiwa kwa kuwa siyo msemaji alisema bado wanafanyia uchunguzi tukio hilo.

Maiti ya msichana huyo imehamishwa Jumapili iliyopita kutoka Hospitali ya Mwananyamala na kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kuhifadhiwa.

STORI: IMELDA MTEMA | UWAZI

Comments are closed.