NAMUONA LULU NDANI YA JENNIFER KANUMBA

KWA wafuatiliaji wa filamu tangu enzi zile ambazo filamu ilikuwa filamu kwelikweli, watakuwa wanamkumbuka vizuri binti mdogo aliyekuwa akifahamika kwa jina la Hanifa Daudi ‘Jennifer Kanumba’. Huyu ni mmoja wa wasanii walioibuliwa na marehemu Steven Kanumba ambapo alikuwa akimtumia kwenye filamu zake mbalimbali akiwa na mwenzake wa kiume anayefahamika kwa jina la Patrick. 

 

Patrick na Jennifer walikuwa ‘mapacha’ ambao ilikuwa wakiigiza filamu na Kanumba ni lazima ibambe. Hii ilitokana na vipaji walivyokuwa navyo watoto hawa.

 

Walikuwa watundu, wabunifu na waliokuwa wakijua kujiongeza wanapokuwa mbele ya kamera. Kutokana na uwezo wao huo, wengi waliwatabiria makubwa. Jennifer na Patrick walionekana kuja kuwa mastaa wa baadaye na hakika Jennifer alikuwa akipita mulemule alimopita staa mkubwa wa filamu Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’.

Kwa wasiofahamu Lulu alianza kuigiza akiwa na umri mdogo sana. Akaonesha uwezo mkubwa hadi leo hii ukiwataja wasanii wanaofanya vizuri kwenye uigizaji Bongo, Lulu hawezi kukosekana. Ndivyo ilivyokuwa ikionekana kwa Jennifer. Bahati mbaya sana ni kwamba, mtu aliyekuwa akiwaongoza kuelekea kwenye mafanikio Mungu aliamua kumchukua.

 

Hapa namzungumzia Kanumba The Great ambaye ndiye aliyewaibua watoto hao, akawashirikisha kwenye filamu zake kama vile This Is It, Big Daddy, Uncle JJ na nyinginezo ambapo kila aliyewatazama watoto aliona kitu kikubwa ndani yao. Bahati nzuri hata wenyewe walipokuwa wakihojiwa walieleza ndoto zao za kuja kuwa waigizaji wakubwa Bongo. Ndoto zao zikazimika baada ya Kanumba kufariki dunia.

 

Nakumbuka wakati Kanumba anafariki, watoto hawa walilia sana. Ilikuwa ni kama wameondokewa na mzazi ama mlezi wao. Yawezekana walikuwa wakililia mengi lakini naamini kubwa lililowaliza ni kwamba nguzo yao waliyokuwa wakiitegemea kwenye sanaa ilikuwa imeanguka. Na kweli, baada ya kifo chake sikuwasikia tena watoto hao. Nilitarajia kuona wasanii waliobaki wakiendeleza vipaji vyao lakini hakuna aliyechukua nafasi ya Kanumba.

Matokeo yake watoto hawa wakapotea. Mara kadhaa walipokuwa wakiulizwa kwa nini wameikacha sanaa walikuwa wakisema kuwa, wameamua kukomalia masomo kwanza, mambo ya sanaa yatafuata baadaye. Yalikuwa ni majibu sahihi lakini ukweli ulibaki palepale kwamba, hawakuwa na mtu wa kuwashika mkono.

 

Kwani enzi wanaigiza na Kanumba hawakuwa wanasoma? Jibu ni Hapana! Lakini pia mbona Lulu alikuwa akiigiza huku akiwa anaendelea na masomo? Mbona wapo wasanii wengi tu ambao licha ya kwamba walikuwa wakisoma lakini waliendelea kufanya sanaa? Maswali hayo yanatufanya mimi na wewe tuhitimishe tu kwamba, kilichowafanya watoto hawa wapotee ni kukosa sapoti kama waliyokuwa wakiipata kutoka kwa Kanumba.

 

Miaka kadhaa imepita sasa, namuona Jennifer ni kama anataka kurudi tena kwenye game. Nimekuwa nikimfuatilia sana kwenye mitandao ya kijamii hasa kwenye ukurasa wake wa Instagram. Anaonekana ni binti anayewiwa kurudi kwenye sanaa. Swali ni je, nani anayeweza kumshika mkono ili kumuendeleza pale Kanumba alipokomea?

Ukifuatilia kwenye ukurasa wake wa Insta utaona kila siku anaposti picha za mapozi mbalimbali kama wanavyofanya akina Wema Sepetu, Irene Uwoya, Jack Wolper na wengineo. Amekuwa mkubwa, amekuwa mzuri, mrembo na anayejitambua kiasi kwamba ukichanganya na kipaji chake anaweza kufaa sana kwenye hizi tamthiliya na filamu zetu. Hakika namuona Lulu mpya kwa binti huyu.

 

Sijui kwa nini nina imani hiyo lakini niweke wazi tu kwamba, mimi nimekuwa mfuatiliaji mzuri sana wa kazi za sanaa za binti huyu tangu enzi zile. Najua uwezo wake, najua anaweza! Swali ni je, bado ana ‘interesti’ ya kuigiza? Je, hali ya soko la filamu kwa sasa inaweza kumfanya aogope kukitumia kipaji chake?

 

Je, anaweza kuiamini filamu kuwa inaweza kuyabadili maisha yake au ana ndoto nyingine baada ya kumaliza shule? Kwa sasa sina majibu ya maswali hayo lakini nikipata bahati ya kuongea naye nitakuwa na lingine la kuzungumza.


Loading...

Toa comment