
NDEGE kubwa ya jeshi la Chile aina ya Lockheed C-130 Hercules imepotea ikiwa na abiria 38 ilipokuwa ikielekea Antarctica.
Ndege hiyo imetoweka jana Jumatatu, Desemba 9, 2019, majira ya wa saa 12:00 jioni kwa muda wa Chile wakati ikipaa kutoka Jiji la Punta Arenas, kwenda katika Kisiwa cha King George huko Antarctica.
Taarifa zinaeleza kuwa ndege hiyo ilikuwa imefika maili 450 kati ya 770 ya safari yake wakati ilipopoteza mawasiliano baada ya kupita Kusini mwa Bahari ya Atlantic na Kusini mwa Bahari ya Pacific.
Kiongozi mkuu wa ndege hiyo, Eduardo Mosqueira, amesema ndege hiyo haikuonyesha dalili zozote za hatari kabla ya kupotea na kuongeza kuwa rubani wa ndege hiyo ana ujuzi mkubwa na ni mzoefu wa muda mwingi, lakini huenda alilazimika kutua baada ya kuishiwa mafuta.
Miongoni mwa waliotoweka na ndege hiyo ni wafanyakazi 17 na abiria 21. Rais Sebastian Piñera amesema juhudi za kuitafuta ndege hiyo na kuwaokoa waliokuwamo zinaendelea.