Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Jully alipompa Ipyana bahasha yenye shilingi laki tatu na kumweleza ampelekee dada aitwaye Milka aliyekuwa anafanya kazi katika ofisi ya kusajili vizazi na vifo iliyopo mtaa wa Makunganya Posta. Je, kilifuatia nini? Songa mbele na utamu huu…
Baada ya dada Jully kumwagiza hivyo Ipyana alimwangalia Nelly na kumwuliza Ipyana kama alikuwa ndugu yake, akamjibu ndiyo.
“Naye upo naye hapa?” aliuliza.
Ipyana alimwambia atakuwanaye ndipo dada huyo aliyekuwa kavaa sketi nyekundu na blauzi iliyokuwa na maua ya rangi mchanganyiko, mavazi yaliyompendeza sana akamkaribisha Nelly.
Nelly aliposema asante, dada huyo alimwuliza Ipyana ndugu yake alikuwa anaitwa nani, akamwambia Nelly, akacheka na kusema makubwa!
“Makubwa gani tena dada?” Ipyana akamwuliza.
“Si hilo jina lake la Nelly? Yeye Nelly mimi Jully haya mdogo wangu karibu sana hapa!” Jully alimwambia Nelly.
“Asante dada yangu, nafurahi kukufahamu,” Nelly alimwambia.
“Mh! Hawa akina dada wa hapa wana mambo balaa yaani kila anayekuona anakushobokea, hongera kaka kwa zali la kupendwa!” Ipyana alimtania Nelly.
Nelly alipoambiwa hivyo kichwa kilivimba kwa sifa akacheka sana, kwa kuwa alikuwa akipenda sana mademu akamwambia rafiki yake lazima atamtafuna mmoja ili kujenga heshima!
Baada ya mazungumzo hayo, vijana hao walikwenda kuosha gari la dada Fatu kwa ushirikiano. Wakati wakiendelea na zoezi hilo Fatu akiwa ofisini akili yake ilikuwa kwa sharobaro Nelly.
Si kwa Fatu tu, hata Jully naye alikuwa kavutiwa na kijana huyo ambaye ndiyo kwanza alimuona siku hiyo, alivutiwa na Nelly kwani alifanana vitu vingi na serengeti boy wake aliyeitwa Peter aliyekwenda kusoma Canada.
“Huyu kijana utafikiria wako pacha na Peter wangu, lazima nifanye kila kitu nimnase kabla hata hajazoeana na wanawake wa hapa maana nawajua kwa kupenda vivulana,” Jully aliwaza bila kujua Fatu naye alimhitaji sana Nelly.
Baada ya kumaliza kuosha gari la Fatu, walikwenda kunywa chai kisha walirudi ndipo Ipyana akamwambia Nelly kwamba amsubiri anakwenda mtaa wa Makunganya alikotumwa.
“Usijali kamanda wangu we nenda, utanikuta,” Nelly alimwambia Ipyana.
Ipyana alipoondoka, Nelly alikumbuka alizima simu muda mrefu akaiwasha, hakukaa hata sekunde mbili Doreen binti wa ushuani aliyekosa raha tangu alfajiri baada ya kumkosa Nelly kisha kuambiwa na fundi Yassin kwamba asingefika site akapiga.
Nelly alipokea simu hiyo, Doreen alipomjulia hali yake alimwuliza alipatwa na masaibu gani yaliyomfanya asifike site, akamwambia ameambiwa asiende.
“Unasemaje d nani kakuzuia?” Doreen alihoji.
Nelly hakuona sababu ya kumficha akamsimulia kila kitu, msichana huyo alisema atafanya kila awezalo Zakayo aondoke pale kama alivyomfanyia mpenzi wake Nelly.
Baada ya kuzungumza kwa muda, msichana huyo alimbusu Nelly na kumuuliza kijana huyo kama alikuwa na nanafasi siku hiyo wakutane sehemu ili wapeane raha.
“Kwa leo haitawezekana mpenzi wangu, nimepata kazi nyingine,” Nelly alimwambia.
Doreen alipoambiwa hivyo alishtuka na kumuuliza alikuwa akifanya kazi gani na wapi, Nelly alimfahamisha kwamba ni kibarua tu huko Posta, msichana huyo akashangaa.
Wakati wapenzi hao wakizungumza Nelly alimuona mama mmoja mtu mzima akija pale walipokuwa wanakaa kusubiri tenda za kuosha magari, mama huyo akamsalimia.
Nelly akiwa ameiacha simu hewani aliitikia salamu ya mama huyo na kumwamkia kisha akamwambia Doreen asubiri atampigia baadaye, msichana huyo aliyesikia wakati Nelly akimwamkia yule mama akasema sawa.
“Ipyana yuko wapi?” mama huyo ambaye licha ya kuwa mtu mzima alionekana alikuwa moto wa kuotembea mbali enzi zake maana aliumbika haswa alimwuliza Nelly.
Nelly alimfahamisha kwamba alitoka kidogo, akamwuliza kama naye alikuwa akishirikiana naye kufanya kazi, Nelly akamwambia ndiyo.
Mama huyo ghafla akatokea kumpenda Nelly kwani ulipita muda mrefu bila kunjunju.
Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo. Maoni tumia namba hiyo hapo juu.