The House of Favourite Newspapers

NEVER GIVE UP YA HARMONIZE NA ELIMU YA KUKATA TAMAA KIBWEGE!

usiku nikiwa ndani ya gari yangu maeneo ya Mwenge jijini Dar kuelekea nyumbani kwangu Goba. Ni eneo linalosifika sana kwa kuwa na foleni hasa nyakati za jioni. Ghafla namuona kijana anakatiza akiwa anauza maji na soda. Anaonekana amechoka sana, naagiza maji ya buku, ananipa kisha yule kijana akarukia gari nyingine kusaka wateja.  Nikiwa nipo kwenye foleni bado nikawa natafakari maisha ya kijana yule. Alionekana ni mwenye kuyahitaji mafanikio kupitia kazi yake ile ya kuuza vinywaji. Kimoyomoyo nikasema kwamba Mungu hawezi kumtupa, kuna siku atayabadilisha maisha yake kama tu hatakata tamaa.

Nikaishia kumuombea dua kisha kuendelea kusikiliza redio. Sikumbuki vizuri ilikuwa ni station gani, mara nikasikia mtangazaji akiutambulisha wimbo mpya wa mwanamuziki Harmonize ‘Konde Boy’. Wimbo unaitwa Never Give Up. Nikajikuta nimesema; whaaaat? Maana nilichokuwa nakiwaza muda si mrefu ndicho kilichokuwa hewani muda huo. Kwa wasiojua maana ya Never Give Up ni usikate tamaa na ndicho nilichokuwa nikimuwazia yule kijana aliyeniuzia maji.

Muda huo gari zilikuwa zimeruhusiwa, ikabidi niongeze sauti ya redio kisha kuusikiliza kwa makini sana wimbo huo. Nikabaini ulikuwa umebeba ujumbe muhimu sana kwa vijana. Harmonize ambaye jina lake kamili ni Rajab Abdul Kahali alikuwa akijaribu kuwasilisha jinsi alivyopambana mpaka kufikia mafaniko aliyonayo sasa. Akawa anaweka wazi kwamba, angekuwa ni mtu wa kukata tamaa, huenda leo hii angekuwa na maisha magumu sana.

Kwamba amepitia vikwazo vingi katika safari yake ya kimuziki, wapo waliokuwa wakimkatisha tamaa kwa kumwambia maneno ya kumvunja moyo lakini kwa kuwa alikuwa anaishi ndoto zake, aliendelea kupambana kuhakikisha zinakuwa kweli. Ndicho kilichotokea!

Yawezekana wapo waliokuwa wanajua mapito ya kijana huyu kutoka kule Umakondeni lakini huenda wapo ambao ni kama mimi kwamba hatujawahi kujua msanii huyu alipita wapi mpaka kuja kuwa Harmonize huyu anayepiga pesa ndefu kupitia muziki. Nasema hivyo kwa sababu, sikuwa na kumbukumbu vizuri kama Harmonize aliwahi kuibukia kwenye mashindano ya Bongo Star Search.

Sasa nilipoona ile clip yake akiwa kwenye usaili wa shindano hilo (sijui ni mwaka gani), ndipo nilipoona ile maana halisi ya kutokata tamaa katika kutafuta kile unachokitaka. Jamaa alienda mbele ya majaji wa shindano hilo ambao ni Salama Jabir, Master J na Madam Ritha huku akiwa na makonfi-densi kama yote.

Akaa-chiwa steji bwana ili aoneshe kipaji chake. Kwa mbwe-mbwe na kujitu-tumua kabisa huku akiona amepata upenyo wa kutoka kumuziki, jamaa si akaanza kuimba ule wimbo wa Malaika. Hakufika hata mbali, majaji Salama na Master J wakamvaa na kuanza kumponda kwamba hajui kuimba, ameuharibu wimbo wa watu. Yaani kwa kifupi alikula za chembe. Walioona ile video watakuwa wanaelewa ninachokieleza hapa.

Kwa kupondwa kule, kwa kijana ambaye alienda kujaribujaribu na wala hakuwa na imani kwamba anauweza muziki, maneno yaliyotolewa na majaji hao yalitosha kabisa kumkatisha tamaa Harmonize na leo hii huenda kama asingekuwa ni kondakta wa basi, huenda ange-kuwa ni mcheza ile ngoma maarufu ya kimakonde ya Singenge.

Lakini kuonesha kwamba alikuwa na imani anaweza kuimba na anaweza kuutumia muziki kuyabadilisha maisha yake, hakukata tamaa. Aliendelea kupambania ndoto yake na leo hii ndiyo huyu tunamuona ana maisha mazuri kuliko hata wale waliomponda kwamba hawezi kuimba.

Maana yake nini? Vijana hatutakiwi kukata tamaa kibwegebwege. Waliofanikiwa ambao unawajua walipitia changamoto nyingi lakini hawakuthubutu kurudi nyuma. Wewe pia unatakiwa kuwa hivyo. Jiamini, pambana huku ukimtanguliza Mungu maana kumbuka mawazo yako anayeweza kuyabariki ni yeye, ukimtupa Mungu wako hata kama utapambana vipi, huwezi kutoboa.

Hili unaweza kuliona kwa baadhi ya watu ambao wao wameng’ang’ania kusaka mafanikio tu, hawakumbuki kwamba kuna Mungu, matokeo yake ni kwamba licha ya kupambana kwao kote miaka nenda rudi wako vilevile. Kwa nini? Kwa sababu wanajiona wao ni wajanja na kufanikiwa kwao ni uwezo wao wakati kuna nguvu nyingine ya ku-weza kufa-nikisha ndoto zao.

Nihitimishe makala haya kwa kumpongeza sana Harmonize kutokana na wimbo wake huo, amethibitisha kwamba kweli yeye ni msanii kioo cha jamii. Naamini atakuwa ametoa fundisho kubwa kwa vijana wengi ambao huenda wanatamani mafanikio kama yake au zaidi. Nimemaliza!!

MAKALA: AMRAN KAIMA

Comments are closed.