The House of Favourite Newspapers

Vilio na Majonzi, Safari ya Mwisho ya Mmiliki wa Super Sami- Picha 11

VILIO, simanzi na majonzi vimetawala kwa mamia ya waombolezaji jijini Mwanza na maeneo jirani wakati wa shughuli ya mazishi ya mfanyabiashara Samson Josia yaliyofanyika eneo la makaburi Itumbili ya wilayani Magu mkoani Mwanza.

 

Mwili wa Samason uliokutwa ukiwa umefungwa kwenye viroba ukielea ndani ya Mto Ndabaka mpakani mwa wilaya za Bunda mkoa wa Mara na Busega mkoani Simiyu juzi, uliwasili asubuhi ya leo Machi 16 ukitokea Hospitali ya Rufaa Mara ulikohifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi tangu juzi.

 

Mamia ya waombolezaji kutoka jijini Mwanza na maeneo jirani amejitokeza nyumbani kwa marehemu wakitumia mabasi ya kampuni aliyokuwa akimiliki Samsoni, Super Sami.

Mabasi ya kampuni nyingine pia yanatumika kusafirisha waombolezaji kutoka jijini Mwanza bila malipo huku eneo la makaburi likifurika waombolezaji wenye nyuso za huzuni, wakilia na kushindwa kuamini kilichompata mfanyabiashara huyo.

 

Marehemu Josia aliyezaliwa mwaka 1968 alipotea tangu Februari 27 mwaka huu kabla ya gari lake aina ya Toyota Land Cruiser kukutwa likiwa limeteketezwa kwa moto ndani ya eneo  la hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara Machi 9.

 

VIDEO: Mazishi ya Mmiliki wa Mabasi ya Super Sami

Ibada ya mazishi inaongozwa na Mchungaji Jackson Meza kutoka Kanisa la African Inland Church of Tanzania (AICT) na kwaya ya kanisa ambayo marehemu alikuwa mfadhili wake ikiimba nyimbo za maombolezo.

 

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara, Jaffari Mohamed, watu wanne wanashikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano kuhusiana na kifo hicho tata kilichoibua hofu na maswali yasiyo na majibu miongoni mwa ndugu, jamaa, marafiki na wakazi wa jiji la Mwanza ambako marehemu alikuwa akiendesha shughuli zake za kibiashara.

Marehemu ameacha watoto sita na wajane wawili.

Picha na Idd Mumba, Global Publishers | Mwanza.

 

UNYAMA! Umeokotwa Mtoni, Mwili wa Mmiliki wa Magari ya Super Sami

Comments are closed.