Nionavyo Mimi: Lazima Serikali Itekeleze Maazimio ya Bunge

MAKALA NA ELVAN STAMBULI | UWAZI |NIONAVYO MIMI

WIKI iliyopita nilisikia bungeni wabunge wakimkumbusha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu maazimio mbalimbali ambayo yalipitishwa na Bunge lakini serikali ikawa kimyaa katika utekelezaji.

Kwa ujumla wapenda haki wengi tulisisimka mwili kwa kukumbuka jinsi baadhi ya watu katika nchi hii walivyofanya ufisadi na kubaki kama walivyo, yaani wanaishi kwa raha mstarehe kana kwamba fedha walizotumia ni zao.

Nikumbushe tu ule ufisadi uliokubuhu ambao ulitikisa na ulifanywa kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na ambao uchunguzi wake ulifichua mengi lakini umechukua muda mrefu sasa kushughulikiwa.

Wakati ule, ndugu zangu, kama mtakumbuka wakati wachunguzi wetu wakikamilisha kupata taarifa za habari hiyo, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alikaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa serikali kwa wakati ule ilikuwa haimtafuti aliyekuwa Gavana wa BoT, Daudi Balali na akasema ikimhitaji itamtafuta na kumpata.

 

Wakati ule hatukupinga kauli yake kwa sababu Rweyemamu yeye alikuwa ni mtoa taarifa tu. Hoja yetu ipo kwa serikali juu ya masuala mbalimbali kwa ujumla yanayogusa matatizo makubwa ya kitaifa hasa ufisadi uliojadiliwa bungeni na serikali kupewa maazimio ili itekeleze.

Hii si mara ya kwanza mimi kama mwandishi wa habari kusisitiza kuwa ipo haja ya kumaliza kero zinazojitokeza ili serikali ipate wasaa wa kushughulikia masuala mengine ya wananchi. Tukirejea namna masuala kama ya EPA, Richmond na sakata la Tegeta Escrow yalivyoshughulikiwa, wananchi wengi hatukuridhishwa.

Tukumbushane tu kwamba Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali iliwataja baadhi ya vigogo waliohusika na kashfa ya IPTL nchini Tanzania akiwemo waziri mkuu wa wakati ule, Mizengo Pinda na kuwataka kuwajibika kisiasa na kisheria, hatukuona hayo yakifanyika.

Sakata hilo la IPTL lilihusishwa na upotevu wa mamilioni ya fedha na kwa muda mrefu ukazuka mjadala mzito katika Bunge la Tanzania.

Katika ripoti hiyo iliyowasilishwa na aliyekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe na makamu mwenyekiti (marehemu) Deo Filikunjombe, ilithibitisha kuwepo mazingira ya udanganyifu na ufisadi katika mchakato wa malipo yaliyofanyika na kueleza kuwa upotevu huo wa fedha ungeweza kudhibitiwa kama kungekuwa na uwajibikaji wa kutosha kwa baadhi ya viongozi.

Kamati hiyo iliwataja viongozi wengine waliotakiwa kuwajibika kutokana na kashfa hiyo kuwa ni mwanasheria mkuu wa serikali, waziri wa nishati na madini, naibu waziri wa nishati na madini pamoja na viongozi wengine wa bodi na katibu mkuu mmoja.

Ripoti hiyo ilitokana na ukaguzi uliofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo ilianika ukiukwaji mkubwa wa taratibu wakati wa uchotaji wa fedha hizo pia mahojiano na mkurugenzi mkuu wa Takukuru na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Waziri Pinda alilimbikiziwa lawama ikidaiwa kuwa alijua kuwapo kwa ufisadi huo na matamshi yake kuwa fedha hizo hazikuwa mali ya umma, wakati aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alionekana na kosa la kutoishauri vizuri serikali na pia kuagiza fedha hizo zitolewe kwenye akaunti hiyo.

Wizarani walikutwa na makosa wengi sina haja ya kuwataja wote.

Kashfa nyingine zilizokuwa nzito katika bunge la Tanzania na kusababisha viongozi kuwajibika akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ni pamoja na kashafa ya Richmond, EPA na sasa hii ya Sakata la Escrow ambayo kwa mara nyingine kamati hiyo ilionyesha wazi mapendekezo yake ya kutaka kuwajibika kwa waziri mkuu, mawaziri na viongozi wengine lakini serikali ikakaa kimya ndiyo maana wiki iliyopita Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akakumbushwa bungeni. Hoja ya awali na inayobaki hadi sasa ni kwamba kuna haja ya kuyamaliza matatizo hasa ya ufisadi kwa wahusika kufikishwa kwenye vyombo husika vya dola ili wabunge na hata sisi wanahabari na hata wanajamii wasiachwe kubaki kutawaliwa na hisia kisha wakalaumiwa kuwa wanajifanya wapelelezi, waendesha mashtaka na mahakimu.

Niliwahi kusema huko nyuma kwamba ukiangalia makosa waliyoyafanya watuhumiwa wengi wa ufisadi wa mali za umma katika nchi hii kwa wataalamu wa sayansi za makosa ya jinai hasa kwa kuzingatia ripoti kwa mfano, za ukaguzi zilizokwishafanywa na kampuni za kitaalamu, haihitaji hata wiki mbili kuwafikisha kortini wahusika.

Lakini kimya na giza nene limetanda, kiasi kwamba mtazamo wa wananchi wengi mitaani na ambao sasa unazidi kupata nguvu kutokana na kigugumizi cha serikali ni kuwa kumbe wenye nazo wako juu ya sheria.

Wanasema hivyo kwa hisia kali za uchungu, wanataka kuona nchi ikisafishwa kwa mafisadi wa fedha za umma nao kuburutwa kortini kwa kutumia sheria zetu. Matokeo ya ukimya na kuahirisha matatizo kunakoendekezwa sasa, ndiyo kunawapa mwanya watuhumiwa wengi kuanza kuja na mikakati, mara vitisho vya kuanika siri nzito za serikali iwapo wataburutwa kortini na pia wengi wao wakiwa na mbinu zinazofanana kwa kutumia utetezi uleule wa jumla; wanapakwa matope na wabaya wao.

Taifa, nionavyo mimi, haliwezi kuendelea kuwa la tetesi hivi, tuhuma zinaibuliwa, uchunguzi unafanyika, inaonekana dhahiri kuna makosa, hatua zinakawia, mitaani zinajaa mijadala juu ya watu, si maendeleo, watuhumiwa nao wanaibua tetesi zenye masi lahi kwao, nchi inakuwa ya tetesi, mijadala na hisia nyingi. Tanzania yenye viwanda haiwezi kufikiwa kwa staili hii. Lazima tubadilike.


Loading...

Toa comment