






BENKI yenye mtandao mkubwa zaidi nchini ya National Microfinance Bank (NMB) leo imewafungulia watoto mbalimbali Akaunti ya Wajibu bila malipo kwa wale waliopata fursa ya kufika kwenye tamasha lilililofanyika katika ukumbi wa Msasani Beach jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo liliandaliwa na Mtangazaji wa Efm, Dina Marious, na kupewa jina la ’Dina Marious Coconut Baby Oil’ ambapo Benki ya NMB ilikuwa imedhamini tamasha hilo lililolenga kuwakutanisha pamoja watoto kusherehekea na kufurahia michezo mbalimbali iliyopo ndani ya ukumbi huo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mratibu wa Elimu ya Fedha wa NMB, Ryoba Mkono, alisema kuwa ni muhimu wazazi na walezi kutumia hafla hiyo kuwafunguliwa watoto wao Akaunti ya Wajibu zitakayowawezesha kutunza akiba kwa ajili ya maisha ya baadaye ya watoto wao.
Akifafanua, Mkono alisema Akaunti ya Wajibu iko katika makundi matatu, moja ni Mtoto Akaunti inayowahusu watoto kuanzia mwaka mmoja hadi miaka 12, ya pili ni NMB Chipikizi inayowahusu watoto wenye miaka 13 hadi 17 na akaunti ya tatu ni Mwanachuo Akaunti ambayo inawahusu vijana kuanzia miaka 18 na kuendelea.
“Ukiwa mzazi au mlezi una wajibu wa kumwandalia mtoto wako mazingira mazuri, ikiwemo ya elimu na maisha mengine ya baadaye kwa kumfungulia Akaunti ya Wajibu,“ alisema Mkono.
Mkono aliongezea kuwa, Akaunti ya Wajibu inampa nafasi mzazi au mlezi kuweka pesa kwenye akaunti ya mwanaye na kila mtoto anapotoa pesa basi mzazi atapata taarifa moja kwa moja kupitia simu yake ya mkononi iliyounganishwa.
Vilevile katika hafla hiyo Mkono alisema kuwa Akaunti ya Wajibu haina makato yoyote na mtoto anapata riba kupitia akaunti yake mpaka asilimia tano na mzazi wa mtoto anaweza kumwekea pesa mtoto katika akaunti yake kupitia NMB Wakala pasipokwenda kwenye tawi au akahamisha fedha kupitia simu yake na ikaingia moja kwa moja. Vilevile watoto waliohudhuria hafla hiyo wamepata fursa ya kuelimishwa juu ya kujiwekea akiba kupitia akaunti zao walizofunguliwa.
NA DENIS MTIMA/GPL
1 Comment